Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558493

Uhalifu & Adhabu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Adaiwa kumchinja mkewe kwa wivu wa mapenzi

Panga Panga

Mkazi wa Kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Mwanaidi Hamisi amefariki dunia baada ya kuchinjwa kwa panga na mumewe, chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo, bila kutaja jina la mtuhumiwa, akisema ni kutokana na wivu wa mapenzi.

Awali, Mkuu wa wilaya hiyo Abdallah Mwaipaya alisema wanandoa hao walikuwa wametengana kwa muda na Alhamisi Septemba 16 mwanaume huyo alimtafuta mkewe na kutaka kutoka naye kwenda kujivinjari na waliporudi nyumbani akamshambulia kwa panga.

Diwani wa Kata ya Kwakoa, Kiembe Mvungi alisema mwanaume huyo alimpigia mkewe simu akimwambia kuna fedha kidogo amepata, hivyo watoke kufurahia kidogo.

“Wakati wakinywa pombe, yule mwanaume alifuatwa mara mbili na mtoto wake wa kiume ambaye si wa mwanamke huyu, akamuuliza baba yake mbona anakaa hadi usiku ule, baba yake akamtaka aondoke akalale,” amesema.

“Yule mtoto alipoamka akaenda kumsalimia baba na baba chumbani. Alipofika mlangoni kwa baba yake akakuta panga lenye damu na kitambulisho na ndani kuna mtu alikuwa amelala na kufunikwa na shuka la kimasai.

Alifikiri ni baba yake amelala hapo, lakini alipofunua shuka akakuta ni yule mamake wa kambo, amekatwakatwa na panga kichwani, mikononi, shingoni na maeneo mbalimbali huku damu zikiwa zimevujia chini,” ameeleza diwani wa kata hiyo.

Alisema baada ya taarifa kutolewa polisi mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Same kuhifadhiwa kwa uchunguzi na taratibu za mazishi, huku muuaji akiendelea kusakwa baada ya kutoweka.