Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 19Article 547468

Habari za Mikoani of Monday, 19 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Aeleza dawa za kulevya zilivyomharibia maisha

Aeleza dawa za kulevya  zilivyomharibia maisha Aeleza dawa za kulevya zilivyomharibia maisha

"NILIANZA kutumia dawa za kulevya mwaka 2006 nikiwa mwanafunzi wa kidato cha nne," anasema Salum Mwakilo, mkazi wa Jiji la Mbeya.

Salumu ambaye sasa ana miaka 26 anasema kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, baba yake alipofariki dunia, mgao wake wote wa mirathi aliutumia kwa ajili ya kujidunga dawa za kulevya.

"Baba alipofariki kama watoto tulipata mgao wa mirathi, mimi nilipata Sh milioni 13. Zilikuwa fedha nyingi wakati huo lakini karibu fedha zote nilizitumia kwenye dawa za kulevya," anasema Salum ambaye alikuwa mraibu wa dawa za kulevya.

Salum ana kumbukumbu inayoumiza jinsi alivyoingia katika uraibu wa dawa za kulevya, hasa anavyoeleza namna dawa za kulevya zilivyoharibu maisha yake.

Anasema wakati ameanza kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, kete ilikuwa ikiuzwa kwa Sh 2,000 na kwamba dawa za kulevya zilikuwa zinauzwa karibu kila mtaa kwa maana kwamba haikuwa shida kuzipata.

Katika kipindi hicho anasema kwa siku alikuwa anatumia wastani wa Sh 50,000 kwa ajili ya dawa tu.

"Nilianza kwa kuchangana kwenye sigara halafu nikahamia kwenye kujipiga sindano, mgao wa mirathi ulipotoka ndio nikawa ninatumia fedha kununua dawa,” anasema.

Salum Mwakilo ni miongoni mwa vijana zaidi ya 300 wanaopata tiba ya uraibu kupitia Serikali na ushirikiano na Shirika la Henry Jackson Foundation Medical Research International (HJFMRI).

Shirika hilo linalojulikana pia kama Walter Reed Program ni Shirika lisilo la kiserikali linalofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia WRAIR-DoD, Ubalozi wa Marekani na limekuwa likitekeleza afua mbalimbali za mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.

Katika mahojiano, Salum anasema: "Makundi ya vijana sio mazuri, unakaa kijiweni mshikaji anakupa sigara uvute kidogo, kumbe sigara imechanganywa na cocaine, ukishatumia lazima baadae utamtafute aliyekupa ile sigara na hapo uteja ndipo unapoanzia."

Anasema aliingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na msongo wa mawazo baada ya baba yake mzazi kufariki.

Anasema dawa za kulevya hazina manufaa kwa mtumiaji kwani mwisho wa siku huwa ni majuto.

Aidha anasema kutokana na uzoefu wake, vijana wengi huingia kwenye kutumia dawa za kulevya kwa kufuata mkumbo, kushawishiwa na hasa wakiwa kwenye msongo wa mawazo.

Anasema unapotumia dawa za kulevya unakuwa na kiu kila wakati na lazima uwe na fedha za kuyanunua na kwamba inafikia wakati wa mtu kushawishika hata kufanya uhalifu ili ipatikane fedha ya kununua dawa.

Anasema maisha ya kutumia mihadarati hayana amani kwani wakati wowote unapokuwa kijiweni unaweza kukamatwa na polisi.

"Unapotumia dawa za kulevya unaona kama zinaweza kukutuliza akili lakini haiwi hivyo, ndio maana wengi unakuta kama wamechanganyikiwa hata nywele hawachani.

"Ukiwa unatumia dawa hakuna anayekupenda, unatengana na familia, kila mtu anakuwa hakutaki, unanyanyapaliwa na jamii, unakuwa hauna makao maalumu, unalala popote," anasema.

Anasema kuna wakati alipata elimu kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kupitia kituo cha waraibu kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya alianza kupata tiba ya Methadone na sasa hatumii tena dawa za kulevya.

"Nimekuwa muelimisha rika, nafundisha vijana wenzangu na kuwapa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa xa kulevya. Sikutegemea kama nitakuja kuoa lakini sasa nimeoa, nina mke na maisha yanaendelea. Nitoe wito kwa vijana wafuate elimu wanayoelekezwa matibabu yapo," anasema.

Mkuu wa Kituo kinachotioa Methadone Mbeya, Dk Elius Bukuku anasema kituo hicho kilianza Julai 31, mwaka 2017 kwa kufungiliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kwamba baada ya kufunguliwa walianza huduma kupitia asasi za kiraia ambazo zimesajiliwa.

Anasema asasi hizo zimekuwa zikiwakusanya vijana na kutoa elimu na kuwaleta kwenye kituo cha kutolea tiba na kwamba mpaka sasa jumla ya waraibu 376 wanakunywa dawa kila siku. Kati yao wanaume ni 360, wanawake 16.

Anasema kituo kinatoa huduma mbalimbali pamoja na kutoa huduma ya kinga na tiba kwa waraibu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, huduma ya kutibu magonjwa nyemelezi kama Kifua Kikuu (TB), magonjwa ya zinaa na magonjwa ya homa ya ini katika Kituo cha MAT, Mbeya.

"Pia tunatoa huduma kinga ambazo ni pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya zinaa, wanawake tunawapa uchunguzi kwa ajili ya saratani ya shingo ya kizazi, virusi vya Ukimwi na dawa kinga dhidi ya TB," anasema.

Anasema miongoni mwa mafanikio ni pamoja na kupunguza kasi ya utegemezi wa dawa za kulevya kwa waraibu na kuwapatia huduma za kuwakinga na matibabu dhidi ya Virusi vya Ukimwi, homa ya ini, kifua kikuu na magonjwa ya ngono.

"Tumewarudisha kwenye jamii yao, wanakunywa dawa na kurudi nyumbani na familia zimeanza kuwarudisha na kuboresha maisha yao kwa ujumla," anasema.

Anasema dawa za kulevya kama heroin kwa kiasi kikubwa inaleta utegemezi na mtumiaji anaendelea kutumia kila mara.

"Asipopata heroin anapata dalili za mwili ambazo hazivumiliki, hawezi kupata usingizi, miayo iliyopitiliza na machozi. Hizo dalili zinafanya aendeleze utegemezi na kujiingiza kwenye matukio ambavyo sio halali kwa jamii," alisema.

Dk Bukuku anasema kwa wanawake matumizi ya dawa za kulevya yanaleta changamoto kwenye homoni za kike ambazo hushuka na kuleta shida kwenye kubeba mimba.

Anasema baadhi ya waraibu wa kike ambao walikuwa wakitumia dawa za kulevya baada ya kutumia tiba ya Methadone kikamilifu sasa wameweza kuwa na watoto.

Anasema katika eneo la Jiji la Mbeya kuna waraibu takribani 600 lakini mpaka sasa ni waraibu 376 tu walikwishafikiwa.

"Dawa za kulevya zinaathiri watu wa makundi yote, walio na elimu na wasio na elimu, wenye fedha na wasio na fedha. Sisi kwenye kliniki yetu tumefanikiwa kuwa na tiba endelevu," anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Henry Jackson Foundation Medical Research International (HJFMRI), Sally Chalamila anasema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu tatizo la dawa za kulevya, kuokoa maisha ya vijana wa Nyanda za Juu Kusini ambapo mpaka sasa wameweza kuwafikia waraibu 376 katika Jiji la Mbeya.

Chalamila anasema wamekuwa wakishirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya pamoja na kudhamini kliniki.

"Kwa kufanya kazi karibu na na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Shirika limekuwa likitoa tiba ya Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU," anasema.

Chalamila anasema Shirika la HJFMRI wanafanyakazi katika mikoa ya Mbeya, Rukwa, Katavi na Songwe na afua ya tohara mkoani Ruvuma.

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene anasema Serikali itaongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya dawa xa kulevya, hususan kwa vijana ambao ni nguvu kazi kwa Taifa.

Akazitaka asasi zisizo za kiserikali zinazofanya kazi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutoa elimu ili jamii isijiingize kwenye matumizi ya dawa hazo ambazo zina athari kubwa.

"Pia Asasi hizo zitoe msaada wa kiuchumi kwa waraibu wanaopata tiba, waangalie kwenye kila mpango wawezeshwe ili wapate shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kuondoa utegemezi,” anasema.

Anaitaka Wizara ya Elimu kuboresha mitaala ili kuwezesha vijana kuata elimu juu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na viongozi wa dini kukemea matumizi ya dawa ya kulevya.

Anasema tatizo la matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa huku bangi ikiongoza kwa kuwa na watumiaji wengi ikifuatiwa na Heroin na Cocaine ambazo huingia kutoka nje ya nchi.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya nchini, Gerald Kusaya anasema mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa kupitia mikakati minne na ushirikiano wa kikanda na kitaifa.

Pia anasema mamlaka imetekeleza mikakati kwa kufanya operesheni ambapo kwa mwaka 2020/2021 mamlaka imeweza kukamata watuhumiwa 12,549 na kati ya hao watuhumiwa 10 wanahusiana na cocaine, 605 heroin, 10,282 bangi, na watuhumiwa 1,555 ni wa mirungi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi anasema athari za matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na wengi wa watumiaji wanapata athari za afya, akili na mwili na hawawezi kuwa na msaada kwa Taifa.