Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 09Article 584416

Uhalifu & Adhabu of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Afia ‘gesti’ akidaiwa kujinyonga na shuka

Afia ‘gesti’ akidaiwa kujinyonga na shuka Afia ‘gesti’ akidaiwa kujinyonga na shuka

Mtu aliyefahamika kwa jina la John Jackson mwenye umri kati ya miaka 20 na 25 amekutwa amekufa kwa kujinyonga na shuka katika nyumba ya kulala wageni.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alithibitisha kuwapo tukio hilo katika nyumba ya kulala wageni ya Amazon iliyopo katikati ya Jiji la Arusha.

Masejo alisema chanzo cha kujinyonga hakijajulikana kwa kuwa hakuacha ujumbe wowote wa maandishi. Mwili umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kusubiri ndugu wa marehemu.

Taarifa kutoka katika nyumba hiyo zinasema mwili uligundulika baada ya mhudumu aliyejitambulisha kwa jina la Eunice Mianga kwenda kufanya usafi saa 5 asubuhi juzi na kujaribu kugonga mlango mara kadhaa bila kufunguliwa.

Eunice alisema mtu huyo alifika katika nyumba hiyo kama mteja wa kawaida na kuandikisha jina kwenye kitabu cha wageni akidai anatokea Mwanza kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro na kupatiwa chumba namba 17.

Alisema baada ya muda, mteja huyo alitoka nje na wakati anarudi alionekana kuwa na chupa ya pombe kali aina ya K Vant na kupitiliza moja kwa moja chumbani kwake.

Hata hivyo, mhudumu huyo alisema asubuhi alienda kumgongea mlango na hapakuwa na dalili za kufungua ndipo alipochungulia kupitia upenyo wa dirisha na kuona shuka nyeupe ikiwa juu na mtu akiwa ananing'inia kwenye dirisha.

“Niliamua kumuita mlinzi na yeye kushuhudia tukio hilo na baadaye kutoa taarifa polisi. Polisi walifika na kuvunja mlango na kutoa mwili wa marehemu lakini katika chumba hicho ilikutwa chupa ya K vant, chupa ya soda aina ya Sprite na dawa ambazo hazikujulikana,” alisema.