Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 08Article 545950

Habari za Afya of Thursday, 8 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Afya wafanikiwa kuondoa kero ya PF3

Afya wafanikiwa kuondoa kero ya PF3 Afya wafanikiwa kuondoa kero ya PF3

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza kumaliza kero za fomu ya PF3 kwa wagonjwa wanaokwenda kupata tiba hospitali ambapo awali walitakiwa kwanza kuwa na fomu hizo ambazo hutolewa Polisi kabla ya kupatiwa tiba.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima alisema hayo juzi usiku akizungumza katika kipindi cha Siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan kilichorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Huduma kwa wateja ndio msingi tangu kushughulikiwa kwa kero ya PF3 hatujasikia kero yoyote”alisema na kuongeza;

“Kingine ni suala la maiti kuchukuliwa hospitali hilo limekwisha ni wachache tu wamebaki na elimu inahitaji kwa watu kufata utaratibu, lakini lingine ni huduma kwa mzee hawasumbuki tena kupata huduma na kupewa kipaumbele na kwa huduma wateja tumetoa namba zetu na tunawasikiliza tumepokea malalamiko 511 kupitia namba 199 asilimia 70 yamefanyiwa kazi na zingine 30 bado yanashughulikiwa”.

Dk Gwajima alisema katika siku 100 serikali pia imetenga Sh bilioni 140 kwa ajili ya mfumo wa bima kwa wote na pia magari 70 ya kubeba wagonjwa yalitolewa na serikali kwa halmashauri na kati ya hayo 20 yalitolewa ndani ya siku 100.

“Ni asilimia nane ya Watanzania wanatumia bima ya afya na mwezi Septemba, 2021 serikali itawasilisha muswaada wa sheria kwa ajili kutoa fursa kwa kila mwananchi kupata huduma za afya ilikizingatia bima ya afya kwa wote na tutangalia kama kuna wale wasio na uwezo serikali itawalipia”alisema.

Dk Gwajima alitaja mafanikio mengine ni kuongezwa kwa dawa mpya zaidi ya 100 kwenye orodha ya dawa zilizokuwa zinatolewa awali.

Alisema katika muda huo serikali iliajiri watu wengi kujaza nafasi za waliostaafu au walioaga dunia.