Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 29Article 566536

Habari Kuu of Friday, 29 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Agizo la Rais Samia kuhusu kesi za mirathi na dhuluma

Agizo la Rais Samia kuhusu kesi za mirathi na dhuluma Agizo la Rais Samia kuhusu kesi za mirathi na dhuluma

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka majaji na mahakimu kukitumia Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri ya Haki za Wanawake kama moja ya miongozo yao katika kushughulikia mashauri ya kutelekezwa, mirathi, dhuluma, udhalilishwaji na unyanyaswaji.

Ameyasema hayo Ikulu mkoani Dar es Salaam wakati akizindua kitabu hicho cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu nchini Tanzania kuhusu haki za wanawake.

Kitabu hicho kimeandikwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linahusika na masuala ya Wanawake (UNWOMEN) na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo (SIDA).

Rais Samia alisema kitabu hicho kimeandikwa na wanachama wa TAWJA waliojitolea ili kuhakikisha kinaakisi matarajio yaliyokusudiwa ikiwemo kutoa rejea rafiki na ya haraka kwa lengo la kuwarahisishia watoa maamuzi katika kulinda haki za wanawake na watoto.

Alisema mwongozo huo utasaidia kuongeza dhamira na nia ya dhati ya kuimarisha mwitikio chanya wa masuala ya kijinsia katika uamuzi wa mahakama na vyombo vingine vinavyoshughulikia utoaji wa haki.

“Kitabu hiki kimekuja wakati mwafaka, wakati ambapo mahakama imekamilisha ujenzi wa kituo jumuishi cha utoaji haki kwa masuala ya familia, wito wangu kwa majaji na mahakimu wanaoshughulikia mashauri ya kutelekezwa, mirathi, dhuluma, uzalilishwaji na unyanyaswaji, kukitumia kitabu hiki kikiwa ni mwongozo miongoni mwa miongozo itakayotumiwa,” alisema Samia.

Alisema lengo la msingi la kitabu hicho ni kuhakikisha utu na heshima ya mwanamke na mtoto vinalindwa na kutetewa na pia kitawapa watoa haki ujasiri wa kutoa uamuzi utakaosababisha kuzika baadhi ya mila, desturi na imani potofu zinazokandamiza na kupoka haki za wanawake na watoto.

Kutokana na umuhimu wake, aliagiza kitabu hicho pia wapewe Jeshi la Polisi katika kitengo kinachoshughulikia kesi za wanawake na watoto na wawapatie mafunzo maalumu, na kitafsiriwe kwa Kiswahili ili watu wengi wakisome.

Alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na TAWJA kwa kuandika kitabu hicho, hajutii kuwa mlezi wao. Alisema historia inaonesha umuhimu wa mwanamke katika kujenga umoja, amani, maendeleo na ustawi katika jamii na taifa, hivyo mchango wake una nafasi kubwa katika uchumi, siasa na mustakabali wa Taifa. “Ikitokea mwanamke anatengwa na kunyanyaswa kwa sababu zozote zile, mfumo wake wa uwakilishi unaingia dosari.

Serikali itaendelea kuielimisha jamii kuhusu haki sawa kwa wanadamu wote na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sheria na utoaji haki ili haki ionekane inatendeka katika nchi yetu,” alisisitiza Rais Samia.

Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Joaquine de Mello alisema kilianzishwa mwaka 2000 na kusajiliwa kama chama cha kijamii na baadaye kikabadilishwa kuwa chama kisicho cha kiserikali na kusajiliwa kikamilifu mwaka jana.

Alisema chama hicho kina jumla ya wanachama 250 wakiwemo majaji na mahakimu wanawake nchi nzima. Alisema tangu kuundwa kwake, uanachama katika chama hicho ni wa hiari na wa kujitolea.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ukurasa wa 168 Ibara ya 120C inahusu kuimarisha mfumo wa wasajili wasaidizi katika halmashauri zote ili kuwezesha uratibu na utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ukiwemo msaada wa huduma za kisheria kwa masuala ya mirathi na ndoa yanayowagusa wanawake na wasichana.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel alisema kitabu hicho ni muhimu kwa kuwa kitawasaidia wanawake kupata haki zao na mwanamke mmoja anaposaidiwa ni sawa na kuisaidia jamii nzima kutokana na umuhimu wa nafasi yao katika jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani, alisema ukatili wa kijinsia unaathiri wanawake duniani kote ikiwemo Tanzania katika nyanja zote za kijamii.

Alisema ukatili wa kijinsia una sura nyingi ikiwemo vitendo vya ubakaji, ukatili majumbani vikiwemo vipigo, mila zinazonyima haki wanawake, unyanyasaji wa kingono, utumikishwaji wa lazima katika vitendo vya ukahaba na ubaguzi wa kijinsia katika maeneo ya kazi, hivyo kitabu hicho kitakidhi lengo lililokusudiwa la kuwa kitabu rejea kwa majaji na mahakimu katika shughuli zao za kila siku kuhusu masuala ya jinsia.

Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg alisema anatumaini kuwa inawezekana kulinda haki za wanawake na wasichana kwa ubora zaidi kupitia utumiaji mzuri wa kitabu hicho.

Mwakilishi Mkazi wa UNWOMEN, Hodan Addou, alisema kitabu hicho cha mwongozo kitasaidia utoaji haki kwa wanawake kuwa kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi.