Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 01Article 567130

Habari Kuu of Monday, 1 November 2021

Chanzo: Nipashe

Agizo la Waziri Mkuu kuhusu nyumba mbovu za serikali

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa ameagiza kufanyiwa ukarabati wa nyumba za Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali likiwemo Shirika la Nyumba la Taifa NHC na kama wakishindwa waziuze kwa wananchi ili zitunzwe vizuri.

Vile vile, amewatwisha mzigo wabunge kushughulikia suala la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo inasababisha nyumba zinazojengwa na NHC kuuzwa kwa gharama kubwa.

Majaliwa aliyasema hayo jana alipokuwa akiweka jiwe la msingi la Mradi wa Nyumba 1,000 Dodoma, zinazojengwa na NHC katika Kata ya Iyumbu na Wilaya ya Chamwino.

“Wizara au taasisi mbalimbali ziweke mipango ya kukarabati na kuboresha nyumba za watumishi zinazochakaa, Shirika la Nyumba mna nyumba nyingi sana nchini, hapa Dodoma mbali ya hizi 1,000 zinazojengwa zipo zile za zamani, lakini sio NHC peke yake na TBA (Wakala wa Majengo) mna nyumba nyingi sana, nyumba nyingi zimechakaa.”

“Nitoe wito kwenu nendeni mkarabati hizo nyumba ziwe kwenye ubora, mmeshindwa kuzitunza ziuze watu waweze kuzitunza nyumba hizo ili mbaki na chache ambazo mtakuwa na uwezo wa kuzisimamia,” alisema.

Alihimiza shirika hilo kuongeza ubunifu zaidi na ubora wa viwango vya nyumba hizo ili ziwe vivutio.

"Nitoe wito kwa taasisi zote zinazojihusisha na ujenzi wa nyumba zihamasishe na kuweka mazingira wezeshi ili wananchi wa maeneo yote nchini wapate makazi kupitia miradi wanayojenga,” alisema.

Aliagiza taasisi hizo zinazojenga nyumba za watumishi na majengo ya umma kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.

“Katika karakana za utengenezaji samani ziboreshwe kimtaji na teknolojia ili kupunguza gharama za uagizaji wa samani nje ya nchi, hapa nimeona mna karakana yenu ya kutengeneza milango na madirisha kwa kuwa nyie mmeamua kuwa na karakana yenu, imarisheni lakini kwa wale wanaotegemea kununua kwenye maduka wakianzisha karakana zao wanarahisisha utendaji na ubora zaidi," alisema.

Alisisitiza miradi ya ujenzi wa ofisi na makazi wigo wake uongezwe nchi nzima na kila idara ijiridhishe kwa kuwa na majengo ya kutolea huduma na NHC ina uwezo wa kujenga.

Majaliwa alisema mradi huo umewezesha kufikia malengo ya serikali ya kutoa ajira kwa Watanzania ambazo 800 zimezalishwa na kuongeza kipato kwa wananchi na kuwataka kuendelea kuchangamkia fursa za ujenzi wa majengo zinazoendelea kwenye maeneo yao.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema nyumba zilizopo Iyumbu zinauzwa na zilizopo Chamwino zinapangishwa na haitakubalika mtu mmoja kununua nyumba zote 300 halafu awe shirika la kupangisha wengine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Dk. Sophia Kongela, alisema ili kupunguza uhaba mkubwa wa nyumba bora nchini, Bodi imejikita kuhakikisha shirika linaongeza uwezo wake wa kifedha ili kujenga nyumba za watu wa kipato cha kati na chini huku akisema VAT kwenye uuzaji wa nyumba unaongeza gharama.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk. Maulidi Banyani, alisema mradi huo utagharimu Sh. bilioni 71 hadi kukamilika na awamu ya kwanza ina nyumba 404 na itagharimu Sh. bilioni 21.4 na hadi kufikia Desemba, mwaka huu, zitakuwa zinakalika.

"Ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa nyumba 1,000 za makazi jijini Dodoma, serikali ililipatia shirika mkopo nafuu wa Sh. bilioni 20 zitakazotumika kama mtaji (revolving fund). Mkopo huu ni wa miaka 15 ambao utalipwa kwa muda wa miaka 12 baada ya miaka mitatu ya kipindi cha ujenzi wa mradi wa nyumba 1,000," alisema.

Pia, fedha za mkopo huo wenye riba nafuu ya asilimia 6.75 zimetolewa na serikali kupitia Benki ya Azania na imekubali kuwakopesha wanunuzi wa nyumba za Iyumbu kwa riba nafuu ya asilimia tisa.

Kadhalika, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kibali cha kukopa Sh. billioni 173.9 ili kukamilisha miradi ya gharama ya juu iliyokuwa imesimama jijini Dar es Salaam.