Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558472

Habari Kuu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Ahadi ya Mfanyabiashara Rugemalira kwa serikali baada ya kuachiwa huru

Rugemalira atoa ahadi kwa Serikali Rugemalira atoa ahadi kwa Serikali

MFANYABIASHARA James Rugemalira, aliyeachiwa huru na mahakama dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi, amemshukuru Mungu kanisani pamoja na serikali na kuahidi kuwa yuko tayari kushirikiana kuijenga nchi.

Rugemalira ametoa shukrani hiyo jana katika misa ya pili aliyoshiriki na familia yake katika kanisa analoabudu la Katoliki Makongo Juu, Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu.

Amesema amesamehe na kazi yake kubwa ni kumwomba Mungu.

Mfanyabiashara huyo ambaye alikaa ndani gerezani kwa miaka minne akisubiri upelelezi wa kesi yake iliyokuwa ikimkabili, alimshukuru Paroko wa kanisa hilo, Joseph Masenge kwa kumtembelea wakati akiwa gerezani na kumwombea.

Katika ibada hiyo ya kushukuru pia, hakuwasahau waumini wenzake kwa kumwombea wakati wote akiwa katika matatizo mpaka alipoachiwa kuwa huru.

Alhamis iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimwachia huru mfanyabiashara huyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya Nole chini ya kifungu cha 91(1) ya kuonyesha hana nia ya kuendelea na mshtakiwa Rugemalira.

Kesi hiyo ilipangwa siku hiyo kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi.

Mfanyabiashara huyo alikuwa mahabusu gerezani kwa takribani miaka minne na miezi mitatu.

Alishikiliwa kwa uchunguzi wa kesi yake tangu Juni, mwaka 2017, alipopandishwa kizimbani kusomewa mashtaka dhidi ya uhujumu uchumi.

Wakili wa Serikali, Grace Mwanga, alidai mahakamani hapo kwamba kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

"DPP hana nia ya kuendelea na kesi hii dhidi ya Rugemalira, tunaiomba Mahakama imwachie," alidai Wakili Mwanga, wakati akisoma maelezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

Katika kuonyesha shukrani kwa Mungu kwa kuachiwa huru, alipotoka mahakamani alikwenda moja kwa moja katika kanisa lake alilokuwa akiabudu yeye na familia yake na baadaye nyumbani kwake.

Katika kesi hiyo Rugemalira alikuwa anakabiliwa na mashtaka 12, ikiwamo la utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.6 na Sh. 309,461,300,158.27.

Katika kesi hiyo pia mfanyabiashara mwingine Herbinder Seth, aliunganishwa katika mashtaka hayo.

Seth aliachiwa huru Juni 21, mwaka huu na kutakiwa kutotenda kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja na pia alitakiwa kuilipa fidia serikali ya Sh. bilioni 26.9 baada ya kuandika barua kwa DPP ya kukiri mashtaka.