Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 18Article 572563

Habari Kuu of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Air Tanzania yaanza safari za DRC

ATCL yaanza safari za DRC ATCL yaanza safari za DRC

Katika jitihada za kuendelea kupanua mtandao wake, Shirika la Ndege la Tanzania limeanzisha safari mpya ya kwenda jijini Lumbumbashi nchini Congo DR kupitia jiji la Ndola Zambia.

Safari hiyo ambayo imezinduliwa leo Novemba 18, 2021 itakuwa ikifanyika mara tatu kwa wiki (Alhamisi, Jumamosi na Jumanne) na inatajwa kuwa itaongeza mapato ya shirika hilo ambalo kwa sasa lina jumla ya safari za nje 9.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, amesema safari hiyo iliyozinduliwa itaongeza biashara katika shirika hilo kutokana na uwapo wa abiria wengi katika safari hiyo na kwamba safari ya kwanza ndege imejaa kwa zaidi ya asilimia 50 kwa tiketi zilizolipiwa.

“Si soko jipya kwa ATCL, ilikuwapo siku miaka ya nyuma na ilikuwa inafanya vizuri kwa kuwa kuna wafanyabiashara wengi wa huko wanatumia bandari ya Dar es Salaam na itakuwa ndiyo safari fupi zaidi kwa ndege,” amesema Matindi na kuongeza kuwa ndege itakayotumika katika safari hizo ni Airbus A220-300.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ambaye alikuwa sehemu ya uzinduzi wa safari hiyo amesema licha mahusiano ya kindugu na kibiashara yaliyopo baina ya Congo na Tanzania, kwa muda mrefu kulikuwa hamna ndege ya moja kwa moja hivyo kuanza kwa safari hiyo kunakuza fursa za kibiashara na kiutalii.

“Safari hii inaandika historia mpya ya kukuza uchumi na utalii katika nchi hizi mbili, hatuna wasiwasi safari hii italeta faida kubwa na huu ni mwanzo. Tumejipanga kuhakikisha shirika letu linafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwa sasa tuna ndege 11 mpaka 2023 tutakuwa nazo 17,” amesema Profesa Mbarawa.