Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 18Article 558235

Habari za Mikoani of Saturday, 18 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Ajali yaua sita, yajeruhi tisa wa familia moja

Ajali yaua sita, yajeruhi tisa wa familia moja Ajali yaua sita, yajeruhi tisa wa familia moja

Watu sita wa familia moja wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia, kupinduka na kutumbukia kwenye bonde lenye urefu wa mita 120.

Wanafamilia hao walikuwa safarini kwenda kwenye shughuli ya kifamilia wilayani Nyasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Joseph Konyo alisema ajali hiyo ilitokea saa 8:30 mchana kijiji cha Kipololo, Barabara ya Mbinga-Lundumato, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma.

Amesema gari hilo aina ya Toyota Coaster mali ya Joseph Eugeni wa Dar es Salaam lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Wilayani Nyasa, lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina la Mohamed Athuman (37), Mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.

Amesema katika ajali hiyo watu waliofariki dunia ni wanawake wawili na wanaume wanne, akiwamo dereva wa gari hilo, wengine ni Penzia Chale (60), mfanyabiashara na mkazi wa Ukonga, Dar es Salaam, Franko Chale (40) fundi magari na mkazi wa Songea Mjini, Joyce Ndonde (45), muuguzi na mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Gerald Ndonde (60), mwalimu wa Shule ya Msingi Ruhuwiko Songea na Jonson Chale (11), mwanafunzi wa shule ya msingi, mkazi wa Dar es Salaam.

Alisema majeruhi waliopatikana katika ajali hiyo walikuwa tisa, kati yao wanaume wanne na wanawake watano ambao ni Nathan ndonde (60) mkazi wa Majumba Sita Dar es Salaam, Godfrey Chale (40), mkazi wa Banana Dar es Salaam, Nelson Ndonde (40) mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Amina Mpangala (34) mkazi wa Dar es Salaam, Janeth Ndonde (35) mwalimu wa Dar es Salaam, Janeth Ndonde (33) mfanyabiashara, mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Olvia Ndonde (36) mfanyabiashara, Mkazi wa Tabata Dar es Salaam.

Wengine ni Catherine Ndonde (45) muuguzi, mkazi wa Dar es Salaam pamoja na Patrick Mpangala (32) mkulima, mkazi wa Tabata Dar es Salaam.

“Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva kwenye mteremko mkali wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1, bila kuchukua tahadhari kwa kuwa alikuwa mgeni wa barabara hiyo, gari lilimshinda na akatumbukia kwenye bonde lenye urefu wa zaidi ya mita 120,” alisema.

Amesema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Mission Litembo, Mbinga, wakipatiwa matibabu na miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Mbinga ikisubiri uchunguzi wa daktari.