Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 585037

Habari Kuu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Ajira za muda za TASAF zaleta manufaa haya

Ajira za muda za TASAF zaleta manufaa haya Ajira za muda za TASAF zaleta manufaa haya

Baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini (Tasaf) katika Manispaa ya Mpanda mkoani hapa waliopata ajira za muda, wamesema ujira wanaopata umewezesha kukidhi mahitaji ya shule kwa watoto wao wanaotarajiwa kufungua shule Januari 17, 2022.

Wamebainisha hayo leo Januari 11, 2022 wakati wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walipokuwa wakipokea fedha za miradi waliyoibua kisha kuitekeleza.

Mmoja wa wanufaika hao aliyejitambulisha kwa jina la Leokadia Kisabo (61), mkazi wa Tambukareli, amesema waliibua mradi wa kukarabati barabara katika mtaa wao na kupata ujira uliomwezesha kukitdhi mahitaji yake. “Tulianza kulima Septemba 2021 leo tumepewa Sh30,000 ambayo nitaitumia kununua chakula na mahitaji ya shule.

“Nina familia ya watu 18 kati yao 11  ni wajukuu, wanaosoma ni wanane. Mimi ni mjane na wajukuu nilionao ni yatima, kabla ya kuingizwa kwenye mpango huu nilihangaika sana, kwani ilifika mahali watoto walilala njaa,” amesema Leokadia.

Naye Mariam Stephen mkazi wa Ilembo amesema anategemewa na wajukuu zake yatima wanne wanaotarajia kuanza masomo ya sekondari 2022.

“Nilikuwa napokea sh25,000 zisizo na masharti zimenisaidia kusomesha yatima. Awamu hii tumelima barabara na nimepata Sh30,000 nitakazotumia kununua mahitaji  ya shule,” amesema Mariam.

Mratibu wa Tasaf Manispaa ya Mpanda, Joshua Sankara amesema walengwa 889 katika mitaa 23 watanufaika na mpango huo, akiongeza kuwa zaidi ya Sh20 milioni zitalipwa kila mwezi.

“Wanalima barabara za udongo, mitaro, vivuko vya miti, kuchimba visima, kuboresha na kupanda miti. Mpaka sasa mabadiliko ni makubwa,” amesema Shankara.

“Lengo la mradi huu ni kuongeza raslimali katika jamii na kuwapa ujira na ujuzi walengwa katika kipindi hiki kigumu,” amesema.