Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 19Article 552466

Uhalifu & Adhabu of Thursday, 19 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Akamatwa kwa utapeli chanjo ya Corona Kilimanjaro

Akamatwa kwa utapeli chanjo ya Corona Kilimanjaro Akamatwa kwa utapeli chanjo ya Corona Kilimanjaro

SERIKALI mkoani Kilimanjaro imemkamata mwananchi (jina linahifadhiwa) aliyejifanya mhudumu wa afya na kuwatoza wananchi fedha kwa ajili ya kupata chanjo ya virusi vya corona.

Mkuu wa mkoa huo, Stephen Kagaigai alisema hayo jana wakati akizungumza na watumishi wa afya wa sekretarieti ya mkoa huo na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi iliyoko mjini Moshi.

Kagaigai alisema serikali imeagiza ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa huo achunguze katika vituo vyote mkoani humo ili kubaini wanaofanya utapeli huo.

Alisema serikali ilitoa maelekezo kwamba chanjo ya Covid-19 inatolewa bure na inahamasisha wananchi waende vituoni kuchanjwa.

"Katibu Tawala shirikiana na timu yako ikiwamo ya afya kufanya uchunguzi wa kina katika vituo vyote vya chanjo mkoa mzima ili kubaini kama kuna watu wanaofanya utapeli kupitia chanjo hii... sisitizeni kuwa chanjo ni bure wananchi waelewe"alisema Kagaigai.

Alitoa mwito kwa wananchi watoe taarifa katika ofisi za serikali ngazi zote wanapobaini matapeli wa chanjo hiyo.

Wakati akizungumza na wananchi waliokwenda kupata chanjo katika hospitali ya Mawenzi, Kagaigai alihimiza watoe taarifa katika vyombo vya dola wanapobaini watu wenye nia ya kutapeli kwa ktumia chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa Kagaigai hadi jana zaidi ya wananchi 21,000 walishapatiwa chanjo mkoani humo.

Kuhusu utapeli wa chanjo hivi karibuni serikali ilionya watu wanaojaribu kujipatia vyeti vya chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 kwa njia za udanganyifu.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alisema wizara inafahamu mfuatano wa namba za chanjo hizo na vituo ambako zimetolewa.

Alisema ikibainika kuwa namba moja imejirudia, watakaoanza kuchunguzwa ni watoa huduma waliotoa namba hizo na wateja wenye vyeti vya namba hizo.