Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 20Article 543460

Diasporian News of Sunday, 20 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Asifu ukomavu wa chama cha ACT-Wazalendo

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amekishukuru Chama cha ACT-Wazalendo kutokana na ushirikiano wanaoendelea kumpa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiserikali tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Aidha alisema mshikamano pamoja na umoja wa wanachama wote wa chama hicho cha ACT Wazalendo unaonesha namna chama hicho kilivyo komaa kisiasa hususani baada ya mchakato uliomfanya yeye kuwa makamu wa Rais kufanyika kwa hali ya umoja.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika Dar es Salaam juzi, Masoud alisema jukumu kubwa alilonalo sasa ni kuhakikisha anatekeleza yale yote kulingana na majukumu yake ya kiserikali ili kukiletea heshima chama hicho.

“Naahidi kuendelea kuitumikia nafasi hii kwa uwezo wangu wote na kwa kiwango bora zaidi ili kufanikisha malengo ya majukumu ninayoyatumikia, kikubwa na zaidi tuendelee kuombeana,” alisema.

Masoud alisema baada ya kufariki kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na kuiacha wazi nafasi hiyo, ACT Wazalendo ilisimama imara bila aina yoyote ya msuguano hadi pale jina lake lilipoteuliwa kushika nafasi hiyo.

“Huo ni ukomavu kisiasa na zaidi kwa kiasi imeonesha chama kipo imara na kinaendelea kusongambele,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Masoud kazi aliyopewa ni nzito hivyo ikitokea amekumbana na changamoto katika utekelezaji wa majukumu hayo basi ijulikane kuwa ni mapungufu ya kibinadamu.

Alisema pamoja na kutumikia majukumu hayo bado ataendelea kukitumikia chama hicho kwa nguvu zake zote na kutimiza malengo ya chama hicho ili kufanikisha azma na malengo yake.