Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 13Article 551308

Uhalifu & Adhabu of Friday, 13 August 2021

Chanzo: Mwananchi

Askari 9 wasota jela miezi miwili kwa mauaji

Askari 9 wasota jela miezi miwili kwa mauaji Askari 9 wasota jela miezi miwili kwa mauaji

Polisi tisa wa Kituo Kikuu cha Wilaya ya Mwanga wametimiza siku 58 mahabusu wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya askari mwenzao wa upelelezi, Linus Nzema aliyepigwa risasi Mei 31 mwaka huu.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, kwa kuwa simu yake ilipokewa na mtu aliyejitambulisha ni msaidizi wake akisema kamanda Maigwa yupo kikaoni. Hata alipopigiwa baadaye, simu yake ilikatwa.

Mwananchi pia lilimtafuta kwa simu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura ambaye alisisitiza atafutwe RPC Maigwa.

Awali, tukio la mauaji hayo linadaiwa kufichwa na polisi kwa kutengeneza hadithi kuwa aliuawa kwa kugongwa na pikipiki ya wasafirishaji mirungi, lakini baadaye ilielezwa aliuawa kwa risasi na si ajali.

Kutokana na taarifa hiyo, Wambura aliunda timu ya uchunguzi iliyothibitisha aliuawa kwa kupigwa risasi, huku bunduki ikiwa ni mali ya jeshi hilo.

Polisi hao kutoka kitengo cha upelelezi, utunzaji silaha na kikosi cha usalama barabarani walikamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Juni 15, 2021 na Julai 15, 2021 kutokana na mauaji hayo yaliyotokea Mei 31. Tukio hilo lililotokea usiku wa manane wakati polisi wa Kituo cha Mwanga wakiwa katika doria ya kupambana na wasafirishaji wa mirungi, lilifichwa.

ADVERTISEMENT “Hawa polisi bado wako mahabusu vituo mbalimbali na ukifanya hesabu kuna ambao wameshafikisha siku 56 leo (jana) na haijawekwa wazi kama court martial (Mahakama ya Kijeshi) ilimaliza kazi yake,” alidai ofisa mmoja wa polisi.

“Utaratibu wa jeshi ni kwamba, ili askari aweze kupandishwa Mahakama ya kiraia ni lazima kwanza ashtakiwe kijeshi na kufukuzwa kazi. Sasa nyie mnachopaswa kuuliza ni kama walishafukuzwa kazi au mashtaka bado yanaendelea,” alidai.

Wakati ofisa huyo akieleza hayo, taarifa nyingine zinadai jalada la uchunguzi wa tukio hilo lilishapelekwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kwa ajili ya kupitiwa na kuona kama kuna ushahidi wa kutosha wa kuwashtaki.

“Katika hili tukio kuna ambaye alifyatua risasi, huyu ni mtuhumiwa muhimu na kuna wengine humo walishiriki kwa namna moja au nyingine kuficha taarifa za mauaji walizozifahamu,” alidokeza ofisa mmoja.

Akitoa maoni yake kutokana na kutofikishwa mahakamani kwa polisi hao kwa wakati, Mwenyekiti wa chama cha mawakili Tanganyika (TLS) Mkoa wa Kilimanjaro, David Shillatu alisema kwa polisi ni lazima wapitie kwanza Mahakama ya kijeshi. “Ingekuwa mtuhumiwa au watuhumiwa ni raia sheria inataka wafikishwe mahakamani ndani ya saa 48 tangu kukamatwa kwao, sasa kwa polisi ni tofauti, maana ni lazima wapitie mchakato huo wa court martial,” alisema Shillatu.

Tukio la mauaji

Tukio la kuuawa kwa polisi huyo lilitokea saa 7 usiku Mei 31, 2021 nje ya baa ya Ndafu katika Kijiji cha Kituri.

Ilidaiwa kuwa aliuawa kwa kupigwa risasi shingoni na polisi mwenzake, lakini polisi wakaficha taarifa za mauaji hayo.

Taarifa ya polisi aliyotumiwa RPC na RCO Kilimanjaro zilieleza kuwa tukio hilo lililofunguliwa jalada la uchunguzi MWG/IR/670/2021 lilitokea saa 7:00 usiku wa Mei 31, 2021 katika Kijiji cha Kituri, Kata ya Kileo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya maofisa wakatengeneza taarifa ya uongo kuwa kifo chake kilisababishwa na kugongwa na pikipiki ya genge la wasafirishaji mirungi, wakichukizwa na kitendo cha polisi kukamata pikipiki yao ikiwa na mirungi.

Inaelezwa kuwa polisi wakiwa doria walikamata pikipiki ambayo haikuwa na plate namba ikitokea Kenya ikiwa imebeba kilo 96 za mirungi na baada ya kusimamishwa na polisi waliokuwa doria, dereva wa pikipiki alifanikiwa kutoroka.