Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540568

xxxxxxxxxxx of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Auawa akijaribu kutoroka Polisi, 25 wadakwa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikiria watu 25 kwa tuhuma za kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani humo na kumuua mtu mmoja anayesadikiwa kujihusisha na masuala ya ujambazi, wakati alipokuwa akijaribu kuwatoroka polisi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo ya Dar es Salaam, Camillius Wambura alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na Operesheni maalumu inayoendelea katika mkoa huo kwa lengo la kupambana na matukio mbalimbali ya uhalifu.

Alisema tukio la kwanza lilihusisha kuuawa kwa ‘jambazi’ aliyejulikana kwa jina la Kilambo Nyabare (44)mkazi wa Chanika anayedaiwa kujihusisha na matukio ya ujambazi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam lililotokea Saa tano usiku Mei 27 mwaka huu.

Kamanda Wambura alisema siku na muda huo, mtuhumiwa alikamatwa na kuhojiwa kisha kukiri kujihusisha na matukio hayo akitumia silaha na kwamba baada ya mahojiano hayo polisi walimtaka kwenda kuwaonyesha mahali alipokuwa ameifukia silaha hiyo na kuongeza kuwa walipofika eneo la tukio jambazi huyo aliwaponyoka na kuanza kukimbia.

“Wakati anakimbia uelekeo wa kwenda maporokomo ya kingo za Bahari Polisi walipiga risasi hewani ili kumuonya asimame lakini hakufanya hivyo na ndipo walipoamua kumpiga risasi ya mguuni iliyomjeruhi na kumfanya kuvuja damu nyingi na ndipo baadae akafariki wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Mwananyamala,” alisema Kamanda Wambura.

Alisema askari walipofukua eneo hilo walifanikiwa kuikuta bunduki moja aina ya shotgun yenye namba S/NO.006074010/CAR 00097133,katika uchunguzi wa awali inaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na washirika wake Aprili 23 mwaka huu walivamia nyumbani kwa kepteni Milton Lazaro, Mstaafu wa JWTZ, Mkazi wa Masaki Dar es Salaam na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo televisheni aina ya LG inchi 49, Laptop aina ya Mac Book air na fedha za Canada dola 2,700 pamoja na silaha hiyo.

Aidha katika tukio jingine Polisi katika Kanda hiyo inawashikilia watu 12 kwa tuhuma za uvunjaji nyumba usiku na kuiba vitu mbalimbali katika maeneo ya Mbweni, Mabwepande, Tegeta na Kawe huku ikiwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa katika matukio hayo kuwa ni pamoja na Tony Peter miaka 25, mkazi wa Tandika Omary Ally (32) mkazi wa Mwananyamala, Karimu Ally (22) mkazi wa Mbezi na Shaibu Salehe (18) mkazi wa Goba.

Wengine ni Bahati Mahame(25) mkazi wa Msasani, Hussein Ally (26) mkazi wa Mkocheni, Kimti Juma (22) mkazi wa Msasani, Abas Athuman (40) mkazi wa Mikocheni, Joseph Saimon (26) mkazi wa Msasani Andrea Moses (25) mkazi wa Msasani, Shabani Omary (18) pamoja na Mohamed Seif (25) wote wakazi wa Goba.

Alisema watuhumiwa hao walipopekuliwa walikutwa na vitu mbalimbali zikiwemo televisheni 13, simu 14, rejeta 3, bampa moja la gari aina ya Marcedes - Benz, kompyuta ya mezani 1, kompyuta mpakato 5, panga moja, jeki ya kuvunjia kisu pamoja na Microwave vyote vikiwa vimeibwa katika matukio hayo.

Katika Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi kanda maalumu Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa saba kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa unyang’anyi majumbani kwa kuwavizia wakazi wanaoishi maghorofa ya Kariakoo maarufu kama ‘panda shuka’ wakati wa mchana au muda wa kazi na kuwafunga wafanyakazi wa ndani, kisha kuwapora fedha na vitu vingine vya thamani.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Athuman (35) Mkazi wa Tandika, Rajabu Bakari(25) mkazi wa Ukonga, Awadh Shaban (26) mkazi wa Ukonga pamoja na Betram Peter(25) mkazi wa Kimara na watuhumiwa wengine watatu ambao kwa pamoja watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili mara upelelezi wa matukio yao utakapokamilika.

Join our Newsletter