Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540559

xxxxxxxxxxx of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Aweso akataa ushemeji miradi ya maji

WAZIRI wa Maji, Juma Aweso amesema ushemeji na ujomba hakuna tena kwenye ukandarasi katika miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.

“Ushemeji, Shemeji sijui Ujomba jomba sasa hakuna, hata ile asilimia 10 hakuna katika Wizara ya Maji, tutachukuliana hatua wenyewe kwa wenyewe, lazima mkubali kubadili mtazamo ili miradi ya maji ilingane na thamani halisi ya fedha inayotolewa na ijengwe kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema

Alisema hayo juzi wakati wa ziara yake katika wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Alisema kwenye sehemu kubwa ya miradi ya maji inayojengwa kazi zimekuwa hazikamiliki kwa wakati.

“Mkandarasi asiyekuwa na uwezo muondoeni na aliye na uwezo ndio afanye kazi,” alisema.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji na majukumu ya Mameneja ni kutatua changamoto na si kusubiri Waziri afike na kutatua changamoto.

“ Fedha mnapewa lazima msimamie watu wapate huduma ya maji, mhandisi wa maji mkoa mnatatuaje changamoto bila kufanya usimamizi na ufuatiliaji?” alihoji.

Aidha alisema wanakwenda kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji .

“Hatuwezi kuona Wizara yetu inakuwa ni Wizara iliyoshindikana,” alisema.

Katika hatua nyingine alimuagiza wakala wa Visima kufika katika wilaya ya Mpwapwa ili kuchimba visima viwili vitakavyoongeza mtandao wa upatikanaji maji na kuwezesha watu wengi zaidi kupata huduma hiyo.

Alisema wilaya hiyo haina chanzo kikubwa, mtandao wa kusambazia maji ni chakavu na sehemu nyingine bado wananchi hawajafikiwa na huduma.

Mbunge wa Mpwapwa George Malima alisema ziara aliyofanya Waziri wa Maji ni ya uponyaji kwani wananchi watapata maji kwa uhakika.

“Hii ni ziara ya uponyaji kila utakachosema wananchi wataamini umeleta maji,” alisema.

Join our Newsletter