Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572947

Habari za Mikoani of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: Habarileo

Baba wa kambo aua watoto wawili wa mkewe

Baba wa kambo aua watoto wawili wa mkewe Baba wa kambo aua watoto wawili wa mkewe

Watoto wawili wa familia moja wameuawa na baba yao wa kambo kwa kuwaziba midomo na kukosa pumzi baada ya kutokea kutoelewana kati yake mkewe ambaye ni mama wa watoto hao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema tukio hilo lilitokea Novemba 17, mwaka huu.

Aliwataja watoto waliokufa ni Lucia Yusufu (6) na Samsoni Yusuf (4) na kwamba tukio hilo lilitokea katika kata ya Usimba, wilaya ya Kaliua, mkoa Tabora

Kamanda Abwao alimtaja mtuhumiwa wa mauaji hayo kuwa ni Nyangwe Chacha (40) na alikuwa akijishughulisha na uganga wa tiba asili na kwamba mbinu aliyotumia ni kuwaziba pumzi ya mdomo na pua hadi kufa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na ugomvi na mke wake ambaye ni mama wa watoto hao aliyemtaja kwa jina la Anastazia Kadamuli (23) mkazi wa Usimba.

Kwa mujibu wa Kamanda Abwao, mtuhumiwa huyo alifika nyumbani akiwa amelewa na kuanza kumpiga mkewe ambaye aliamua kukimbilia kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Mtakuja kilichopo kijiji cha Kazaroho .

Alisema tukio la kipigo lilifanyika Novemba 16, mwaka huu na kumsabishia mwanamke huyo kulala nyumbani kwa mwenyekiti kwa ajili ya usalama wake.

Kamanda Abwao alisema Novemba 17, mwaka huu mwanamke huyo aliporudi nyumbani alikuta watoto wake wameuawa kisha kuzikwa ndani ya nyumba hiyo na kuanza kupiga kelele kuomba msaada.

Aalisema mtuhumiwa alitoroka baada ya kufanya tukio hilo na juhudi za kumsaka zinaendelea, huku watu wawili wakishikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na tuko hilo la mauaji.

Miili ya watoto hao ilifanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko rasmi.