Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 05Article 545497

Habari za Mikoani of Monday, 5 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bandari Dar yavunja rekodi siku 100 za Samia

Bandari Dar yavunja rekodi siku 100 za Samia Bandari Dar yavunja rekodi siku 100 za Samia

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema mkoa wake umefanya vizuri katika ukusanyaji mapato katika siku 100 tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani.

Makalla aliyasema hayo juzi usiku katika Kipindi cha Siku 100 za Rais Samia Suluhu kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alisema baada ya Rais Samia kuagiza akaunti za wafanyabiashara zilizofungwa zifunguliwe na kupiga marufuku kubughudhiwa kwa wafanyabiashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam imekusanya Sh trilioni 3.8 sawa na asilimia 89 ya malengo.

Kwa mujibu wa Makalla, katika siku hizo 100 manispaa tano za Mkoa wa Dar es Salaam zimekusanya Sh bilioni 40.3.

Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, alisema makusanyo ya Mei yalifikia Sh bilioni 84 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa.

Makalla alitaja baadhi ya changamoto katika mkoa huo kuwa ni pamoja na ufanyaji biashara kiholela bila kuzingatia usafi na kwamba, ofisi yake inaandaa mpangokazi ili kukabili tatizo hilo.

Alitaja changamoto ya pili kuwa ni ukosefu wa vifaa kwa wanaoshinda tenda za kufanya usafi katika jiji.

"Changamoto ya tatu ni kutosimamia sheria zilizowekwa ili kuhakikisha usafi unazingatiwa, hapa tutahakikisha sheria zinazingatiwa na kama halmashauri haina sheria za usafi, watunge haraka ili Dar es Salaam iwe safi," alisema Makalla.

Aliitaja changamoto ya nne kuwa ni mwamko mdogo wa wananchi kulipa ada za taka hali inayosababisha mlundikano wa takataka kwenye maeneo mengi.

Makalla alisema hadi sasa hakuna elimu ya usafi kwa wananchi kuwahamasisha wazingatie usafi kuanzia katika makazi yao na mazingira yanayowazunguka.

Changamoto nyingine kwa mujibu wa Makalla ni utoaji wa mikataba mifupi kwa kampuni za usafi hivyo kuwanyima fursa ya kupata mikopo katika benki au taasisi nyingine za fedha.