Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 27Article 559774

Habari Kuu of Monday, 27 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Benki ya Dunia imefadhili miradi ya trilioni 11.058/- Tanzania

Benki ya Dunia imefadhili  miradi ya trilioni 11.058/- Tanzania Benki ya Dunia imefadhili miradi ya trilioni 11.058/- Tanzania

SERIKALI inatekeleza miradi yenye ufadhili wa Benki ya Dunia yenye thamani ya Sh trilioni 11.058.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo jana mkoani Singida alipokuwa akitoa taarifa ya wiki ya serikali.

Alisema ufadhili wa Benki ya Dunia unatokana na kuwapo ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na taasisi hiyo ya fedha.

"Niwape ujumbe kutoka kwa Rais kuwa yeye ameamua Tanzania iende pamoja na nchi nyingine duniani na Tanzania iko tayari kushirikiana nao na mataifa yote aliyokutana nayo Mheshimiwa Rais yamemhakikishia kuwa watashirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwamo za maendeleo," alisema Msigwa.

Alisema akiwa Marekani, Rais Samia alikutana na Rais wa Benki ya Dunia ambaye aliahidi kuongeza ushirikiano katika miradi nchini.

Msigwa alisema kwa sasa Benki ya Dunia inafadhili miradi inayoendelea kutekelezwa nchini yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 4.808 sawa na Sh trilioni 11.058.

Alisema miradi hiyo ipo katika maeneo ya miundombinu ya barabara, umeme vijijini, maliasili na utalii, uvuvi, maji na mpango kabambe wa kuifanya Tanzania ya Kidijitali.

Alisema pia Benki ya Dunia inafadhili miradi tisa ya kimkakati inayohusisha Tanzania na nchi majirani kupitia mpango kabambe wa kuzisaidia nchi masikini (IDA).

Msingwa alisema kupitia mpango huo, Benki ya Dunia imetoa dola za Marekani milioni 697 sawa na Sh trilioni 1.2 kugharamia miradi ya uvuvi, nishati, elimu ujuzi na kujenga njia za umeme.

"Mheshimiwa Rais hakwenda Marekani kutembea, amefanya kazi kubwa pamoja na kuhudhuria mikutano kama mitatu hivi, pia amekutana na viongozi mbalimbali na kuyajenga," alisema Msigwa.

Alisema Rais Samia alikutana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michael na baraza hilo likaeleza kuwa lipo tayari kuisaidia Tanzania kupanua huduma za afya na kukabiliana na Covid-19 hasa kupata vifaa tiba.

Alisema Rais pia alikutana na Mkurugenzi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) ambao nao walikubali kuongeza ushirikiano na Tanzania na katika kutafuta masoko.