Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 04Article 545206

Habari Kuu of Sunday, 4 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bilioni 570/- kunufaisha wanafunzi 160,000

Bilioni 570/- kunufaisha wanafunzi 160,000 Bilioni 570/- kunufaisha wanafunzi 160,000

SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga kutumia kiasi cha bil 570/- katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo zaidi ya wanafunzi 160,000 watafufaika.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kiwango cha fedha kilichotengwa kimevunja rekodi katika miaka 16 ya uhai wa HESLB.

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, kati ya wanafunzi hao 160,000, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa 62,000 wakati wanaoendelea na masomo watakua 98,000.

“Niwaibie siri tu. Hadi mwezi uliopita, bajeti ya mikopo ilikua bil500/-. Lakini katika siku zake 100 za uongozi kama Rais wetu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza bil70/- na kufikia hizi bil 570/- kwa mwaka 2021/2022 sawa sawa na ongezeko la bil106/- (sawa na asilimia 22.8%)” alisema Prof. Ndalichako.

Aliongeza kuwa ongezeko hilo linathibitisha nia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuwawezesha vijana wengi kupata fedha na kusoma ili watumikie nchi yao na kuwataka waombaji wahitaji watulie, na kusoma maelekezo na kuomba kwa usahihi ili watimize ndoto zao.

Katika mwaka wa masomo wa 2020/2021, Serikali imetenga na kutoa bil464/- zinazowanufaisha jumla ya wanafunzi 149,398. Kati yao, wanafunzi 55,287 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 94,111 ni wale wanaoendelea na masomo.

Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako aliitaka HESLB kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa waombaji ili waweze kuelewa sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwasaidia vijana wengi wanaoomba mikopo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema wamepokea maelekezo na kuanzia Julai 12 mwaka huu, maafisa wa HESLB wataanza kuendesha programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi chini ya kampeni ya #WeweNdoFuture.

“Tunakamilisha utaratibu na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili tuwafikie vijana wote waliopo katika kambi 19 za JKT kuanzia Julai 12 … tutaendesha pia programu hizi kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii na mikutano na wadau,” amesema Badru.