Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 20Article 552547

Habari Kuu of Friday, 20 August 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Bunge kufanya marekebisho sheria ya "Tozo za Miamala"

Bungeni Dodoma Bungeni Dodoma

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema Bunge liko tayari kufanya marekebisho yatakayohitajika kwenye tozo za miamala ya simu zilizopitishwa wakati wa mkutano wa Bunge uliopita.

Aliyasema hayo jana jijini hapa alipofungua kongamano la walimu wenye ulemavu nchini lililoandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

"Tulipitisha suala la tozo ya miamala, kwa kweli ndugu zenu wawakilishi hatujapitisha kitu kile kumkomoa mtu yeyote, tumepitisha kwa nia njema kabisa.

"Labda katika nia njema ile kuna maeneo hatukuangalia vizuri, basi tutajaribu kutizama vizuri huko tunapokwenda kama Rais Samia alivyoelekeza.

“Kwa hiyo, mtaona hili jambo la tozo kwa nini tulilijadili sana sana tukaona twende njia hiyo, kama nilivyosema panapohitaji kupiga pasi kurekebisha tutafanya hivyo, ila tukiondoa tozo tumeacha gizani yale malengo yetu yote tuliyotaka kufanya, tutakwama.

“Ila unaweza rekebisha kidogo, kwa mfano unaweza kumbakishia anayetuma akakatwa lakini anayepokea apokee taslimu au tunaweza rekebisha viwango kidogo kama vimezidi sana, basi tukavirekebisha rekebisha lakini kwa kweli kimsingi tozo watu wasipotoshe, ni kitu muhimu sana kwa nchi yetu,” alisema.

Alibainisha kuwa dhamira ya Bunge kupitisha tozo hizo ni kupata fedha zitakazoelekezwa kusaidia ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Spika Ndugai alisema kuwa ndani ya miaka mitano, serikali imepanga kukusanya Sh. trilioni tano ambazo zitatumika katika ujenzi huo wa madarasa pamoja na kusaidia mikopo ya elimu ya juu.

“Bunge litaendelea kujadili suala la tozo kama Rais alivyoelekeza lakini tulifanya hivyo kwa manufaa ya taifa, kwa sababu tunahitaji kuona madarasa ya shule za vijijini yawe kama ya mjini," alisema.

KURA VITI MAALUM

Kuhusu upatikanaji wa wabunge wa viti maalum, Spika Ndugai alisema ni vyema uwapo mfumo wa wabunge hao kupatikana kwa kupigiwa kura na wananchi moja kwa moja badala ya sasa ambapo wanachaguliwa kupitia makundi maalum.

"Tukienda nchi za wenzetu tunapata shida, tunaulizwa maswali kuhusu tofauti ya wabunge wa viti maalum na wabunge wengine ikoje, unakuta mtu anatuuliza hivi bungeni kuna viti aina mbili.

"Pale bungeni tuna kundi linawakilisha wenye ulemavu Tanzania, bahati mbaya au nzuri wanatoka kwenye kundi la lile viti maalum CCM kwenye kundi la wanawake.

"Hatujaweza kuwa na mfumo mpaka sasa wa kuwa na wawakilishi wa wenye ulemavu wa moja kwa moja wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi.

"Kwa hiyo huko mbele kwa sababu nchi inabadilika na mambo yanabadilika, ninafikiri muwe mnafikiri namna gani siku moja tunaweza kuwa na wawakilishi ambao wamechaguliwa na wenye ulemavu wenyewe kwa upana wake wa kura moja kwa moja sio kwa kupitia vyama.

"Tufikirie ni namna gani tunaweza kupata wawakilishi wetu kwa kuwapigia kura kama wengine na sio wenye ulemavu peke yake, tungependa hata wawakilishi wetu wanawake wasiwe hili neno viti maalum, lingeondoka. Kwa nini liwe viti maalum?" alihoji.

Kuhusu chanjo ya UVIKO-19, Spika Ndugai alisema yale yanayotokea bungeni waachiwe wenyewe, Bunge litajua, akisisitiza walimu wakachanje chanjo hiyo kwa kuwa kupoteza mwalimu mmoja ni pigo kwa taifa.

Alishauri walimu kujishughulisha kiuchumi ili kuepukana na mikopo umiza ambayo inawafilisi kwa kuweka kadi zao za benki kama dhamana.