Uko hapa: NyumbaniInfos2019 11 15Article 488065

General News of Friday, 15 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Bunge la Tanzania lapitisha azimio la kumpongeza Spika Ndugai

Bunge la Tanzania lapitisha azimio la kumpongeza Spika Ndugai

Dodoma. Wabunge wa Bunge la Tanzania leo Ijumaa Novemba 15, 2019 wamepitisha azimio la kumpongeza Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai kwa kuwezesha utekelezaji wa Bunge Mtandao (e parliament).

Akisoma azimio hilo, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Bunge, Mary Chatanda amesema utekelezaji wa dhana hiyo unatarajia kuleta manufaa makubwa kwa Bunge letu na Taifa kwa ujumla.

“Utasaidia kuokoa gharama kubwa iliyokuwa inatumika katika kuandaa na kuzalisha nyaraka na taarifa mbalimbali zinazohusiana na shughuli za Bunge,” amesema.

Ameipongeza pia Sekretarieti ya Bunge chini ya usimamizi wa Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai kwa jinsi walivyojitoa na kufanikisha utekelezaji wa maelekezo ya Spika na Tume ya Utumishi wa Bunge kwa ufanisi, muda mfupi na kwa gharama nafuu.

“Katika hali ya kawaida usimikaji wa mifumo ya kimtandao ungeweza ukafanywa kwa kutumia wataalamu wa nje chini ya kampuni binafsi na kwa gharama kubwa,” amesema.

Hata hivyo, amesema watumishi wa Bunge kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (e Government) wameweza kufanikisha suala hilo kwa wakati na kwa ufanisi.  

Amesema matumizi ya mfumo huo yanalifanya Bunge la Tanzania kwenda na wakati na kuendana na uendeshaji wa mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola ambayo yameshaanza kutumia mifumo kama hiyo.

Azimio hilo liliungwa mkono na wabunge Azzan Zungu (Ilala-CCM) , George Lubeleje (Mpwapwa-CCM), Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF) ambaye alishauri mwakani vishikwambi hivyo pia viweze kutumika nje ya  Bunge.

Join our Newsletter