Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 29Article 544636

Habari Kuu of Tuesday, 29 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Butiku akerwa ukosoaji viongozi usiozingatia tija

Butiku akerwa ukosoaji viongozi usiozingatia tija Butiku akerwa ukosoaji viongozi usiozingatia tija

MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku ameonya dhidi ya kasumba ya baadhi ya watu kutaka kuendeleza malumbano na kukosoa utawala wa viongozi wakuu wa nchi, bila kuzingatia maslahi ya nchi.

Ametaka malumbano ya kutaka kulinganisha nani bora baina ya viongozi yaachwe mara moja na badala yake, nguvu zielekezwe kumsaidia Rais Samia Suluhu kutimiza majukumu yake kuwahudumia Watanzania.

Alibainisha hayo Dar es Salaam juzi wakati akichangia mjadala katika Kongamano la Siku 100 za Rais Samia lililofanywa na wadau wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC).

Akizungumzia siku 100 za utawala wa Rais Samia, Butiku alisema rais kafanya mengi mazuri na amefanikiwa kwa sababu hakusilikiza maneno ya uchonganishi yanayotolewa na baadhi ya watu wanaolenga kuvuruga nchi.

"Rais kafanya mengi sana, na kaweza kwa sababu hakusikiliza maneno ya uchonganishi; sasa hao wanaoendeleza debate (mijadala) nani kiongozi bora, tuache kuanzia leo; na kama ni madhambi nani hanashambi, Waziri Mkuu tusaidie tuache hayo mambo ili tufocus (kuangalia ) mbele," alisema Butiku

Alisema kwa sasa watu wote wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na wengine ni sawa chini ya uongozi wa Rais Samia na mchango wa kila mmoja katika ujenzi wa taifa unathamniwa.

"Sote ni sawa; twende pamoja kuwezesha kila mmoja ashiriki, tumsaidie Mama (Rais Samia) kutimiza hayo bila kutugawa ili watu wote waweze kujihudumia na kuhudimia wengine," alisisitiza.

Katika kongamano hilo, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu, alimsifia Rais Samia kwa kutatua kero na kuleta watu pamoja ndani ya siku hizo 100 za utawala wake.

Kazungu alisema awali Kenya na Tanzania zilikuwa na kero 64 za kibiashara, lakini ndani ya siku 100 za uongozi wake, amefanikisha utatuzi wa kero 30 na zilizobaki ametoa miezi mitatu ziwe zimetatuliwa.

"Siku 100 za Rais Samia ndizo zinatoa mwelekeo wa uongozi wake ni upi, tunayoyaona yanatia moyo sana kwa sababu ndani ya muda mfupi tumefanikiwa kuondoa kero nyingi na imani yetu nchi hizi mbili ni ndugu zitamaliza kero zilizobaki kwa sababu maagizo yameshatolewa kwa watendaji kuzishughulikia," alisema Balozi Kazungu.

Naye Waziri Wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema kauli za Rais Samia kuhusu masuala ya fedha, zinatengeneza nguvu kubwa ya fedha kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mwigulu, miradi ya maendeleo vijijini imepewa Sh trilioni tatu hali itakayofungua milango ya fedha kwa wananchi.

"Rais ameturahisishia kazi; sasa kazi ni sisi sote mkiwemo nyie sekta binafsi kufuate sheria. Tutende haki ili kodi ikusanywe kwa hiari na kusaidia hiyo miradi ya maendeleo kutekelezeka,"alisema Mwigulu.

Akihitimisha kongamano hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwaagiza watendaji wote kuanzia wakuu wa wilaya, mikoa hadi wizara kuhakikisha wanatekeleza maazimio ya mkutano huo wa TNBC ili kuleta tija kwa taifa.