Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 28Article 544537

Siasa of Monday, 28 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM: Dini zinaimarisha amani, umoja nchini

CCM: Dini zinaimarisha amani, umoja nchini CCM: Dini zinaimarisha amani, umoja nchini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinatambua na kuthamini mchango wa dini zote katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo jana Tanga katika Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

Shaka alikuwa akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.

Alisema kazi ya kulinda na kuitunza amani ya nchi ni jukumu la kila raia mwema, hivyo wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuvipa taarifa kuhusu uwepo wa mipango au viashiria vya kuhujumu amani na usalama.

Shaka alisema CCM kinawaomba Watanzania kuendelea kutunza, kuilinda na kudumisha amani kwa vile maendeleo hayawezi kupatikana bila amani.

"Mwenyezi Mungu katika Quran Suratul al Imran (103) amesema shikamaneni katika kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msifarikiane kumbukeni neema ya Allah iliyo juu yenu. katika Zaburi 133 (1), anasema tazama ilivyo vema na kupendeza, ndugu wakae pamoja kwa umoja,” alisema.

Akaongeza: “CCM kinaipongeza serikali inayongozwa na Rais Samia kwa namna inavyoendelea kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi za kisiasa, kiimani na kikabila."

Alisema CCM kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, itaendeleza amani, umoja, usalama, utawala bora wa sheria na utulivu wa kisiasa jambo litakalowezesha shughuli zote za kiimani na kimaendeleo kufanyika nchini.

"Niwaombe Watanzania wote tuendelee kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan na serikali anayoiongoza kuendelea kutuongoza kwa kuheshimu utawala wa sheria, haki na usawa ili amani yetu iendelee kudumu na nchi yetu ipige hatua zaidi kimaendeleo," alisema Shaka.

Mkutano huo ulifunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.