Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 17Article 547306

Siasa of Saturday, 17 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM: Hatuuchukii upinzani

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi (NEC) ya CCM,  Shaka Hamdu Shaka Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitahasimiana na upinzani kwa kuwa kuwepo kwao ni tija na neema kwa chama hicho tawala ili kubaini kasoro, hitilafu na upungufu wao waweze kujirejebisha na kujipanga vizuri zaidi na kuendelea kubaki madarakani, japo ukosoaji mwingi hauna mashiko.

Chama hicho kimesema ni uongo kudai kuwa chama tawala kinaukandamiza upinzani kwani uwepo wake kumeiwezesha CCM kujisahihisha na kujipanga kimkakati na kisera kila inapoona kuna hoja ya maana na haja ya kufanya hivyo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Konde kisiwani hapa.

Alisema CCM inapenda upinzani uwapo ili kukifanya kuona makosa yake na kujirekebisha na kujiimarisha zaidi.

“Hata ripoti ya Jaji Francis Nyalali iliposema watu asilimia 80 walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee, CCM iliamua kusimama upande wa asilimia 20 ambayo ilitaka vyama vingi. Kama CCM ingechelewa kupitisha maamuzi hayo yasingetokea mabadiliko ya kisiasa nchini.”

“CCM haiko tayari kuona upinzani ukidhoofika na kufa kwa sababu hakuna mtu mjinga anayeweza kukubali kukivunja kioo chake cha thamani anachokitumia kwa ajili ya kujitazama kabla ya kuvaa ili ajipime namna alivyopendeza kabla kutoka kwenye jamii,” alisema.

Shaka alisema upinzani utaendelea na kazi ya kuisafishia njia CCM ili ifikie malengo yake, kwani haujakidhi viwango ili Watanzania wengi wakubali kuwapa dhamana ya utawala wan chi wakati hawajakomaa na hawajajijenga kitaasisi.

"Mchagueni Shekha Mpemba Fakhi akaungane na Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi katika kuwaletea wana Konde maendeleo ya ukweli. Konde inahitaji mtu makini, jasiri, shupavu na aliye na utayari wa kuwavusha, msihangaike na wagombea wa upinzani ambao watawatelekeza kwa kubeba ajenda zao badala ya ajenda za wananchi, hii ni kwa sababu Ilani iliyo katika utekelezaji ni ya CCM kikiwa ndio chama kinachounda serikali,” alisema Shaka.

Katika mkutano huo wa kufunga kampeni ubunge Jimbo la Konde, mgeni rasmi alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na uchaguzi huo mdogo wa ubunge utafanyika kesho.