Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 12Article 546613

Habari Kuu of Monday, 12 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM: Maji safi, dawa si anasa

CCM: Maji safi, dawa si anasa CCM: Maji safi, dawa si anasa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwa hali inavyokwenda nchini kunataka kujengeka tabia ya kuonekana kuwa dawa na maji safi kwa wananchi ni suala la anasa wakati ni mahitaji muhimu kwa uhai wa maisha na uchumi.

Kimesema changamoto za upungufu wa dawa, maji safi na salama na wawekezaji kucheleweshewa huduma za msingi kwa ajili ya uzalishaji zimebainika kuwa mambo ambayo CCM haiwezi kuyavumilia.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo alisema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake na sekretarieti mkoani Songwe.

Chongolo alisema wananchi wanalipa kodi na wanachangia huduma hizo hivyo haiwezekani waliopewa dhamana wasiwasikilize na kufanya bidii ya kutatua kero.

“Kote tulikopita kilio ni dawa na maji safi, naomba niwahakikishie ndani ya wiki moja baada ya kurejea Dodoma nitaziita wizara zote zinazohusika kutueleza hili limekaaje maana serikali inatenga mabilioni ya fedha na kila wakati kauli za tunazo dawa za kutosha zinatolewa wakati haziakisi uhalisia kwenye maeneo ya huduma kwa wananchi.

Tunataka kujua tatizo ni nini, ili kutatua changamoto hii. Vivyo hivyo kwenye maji safi”alisema.

Chongolo aliwataka wataalamu wa halmashauri zote wahakikishe wanapoibua miradi ya kimkakati yenye kulenga kusisimua uchumi na kuongeza mapato kwenye maeneo yao wahakikishe wanazingatia mahitaji na matakwa halisi ya watumiaji wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“Unapenda kubaki au kuendelea na cheo au dhamana uliyoaminiwa timiza wajibu kwa kuhakikisha wananchi wanaona fahari ya wewe kuwepo katika nafasi uliyopo vinginevyo hatutakubali kukuona hapo wakati unatugombanisha nao, hii ndio kazi ya CCM,” alisema.

Chongolo alitoa mfano wa kujenga mradi wa soko la ghorofa halafu akina mama wanaouza mbogamboga wanawekwa ghorofa ya kwanza na hakuna eneo la bodaboda, bajaji, machinga na mama/baba lishe kufanya shughuli zao.

“Hakuna raia wa daraja teule, sote tuna hadhi sawa. Miradi hii izingatie mahitaji na mazingira halisia ya watumiaji ili kuimarisha mnyororo huo wa uchumi,”alisema Chongolo.

Katibu Mkuu wa CCM na Sekretarieti yake jana walitarajia kuanza ziara mkoani Mbeya.