Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 06Article 541249

Siasa ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM YAIPA SERIKALI MAELEKEZO 7

CCM YAIPA SERIKALI MAELEKEZO 7 CCM YAIPA SERIKALI MAELEKEZO 7

CHAMA Cha Mapinduzi CCM kimetoa maelekezo saba kwa Wizara ya Fedha na Mipango ya kuzigatia wakati wa bajeti yake ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Miongoni mwa maelekezo hayo ni kuimarisha na kuwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina kusimamia mashirika ya umma yazalishe kwa faida na kutoa mchango kwa maendeleo ya Taifa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Shaka Hamdu Shaka, imetaja mashirika yanayohitaji usimamizi ni pamoja na Shirika la Reli (TRC), Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la Ndege (ATCL) pamoja na Kampuni ya Simu (TTCL).

Shaka katika taarifa hiyo, ametaja mambo mengine ambayo serikali kupitia wizara hiyo ya fedha inapaswa kuzingatia, ni kuhakikisha uchumi unakua hadi asilimia nane, mfumuko wa bei usivuke tarakimu moja na kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kutekeleza sera ya kujitegemea.

Mengine ambayo chama kimeielekeza serikali ni kuhakikisha deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu huku kikisisitiza nchi kuchukua mikopo yenye tija isiyoathiri uhimilivu wa deni, mifuko ya utoaji wa mikopo kwa wananchi iimarishwe na fedha zinazoidhinishwa kwenye bajeti zipelekwe kwa wakati.

Shaka alisema Wizara ya Fedha na Mipango ndicho kitovu cha mipango ya maendeleo na inahusika na uwezeshaji wa rasilimali fedha kwa wizara nyingine zote.

Alisema wizara hiyo inatakiwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 fungu la 18 linalotaja kuwa uchumi wa nchi unakua wa kisasa, shirikishi na shindani ambao ni wa kukuza viwanda vidogo vya kati na vikubwa.

“Katika kuhakikisha malengo hayo, chama kimeielekeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango katika bajeti hii,kwa kuhakikisha wizara inakuza uchumi kwani kwa mwaka wa fedha 2020/2021, ukuaji wa uchumi umekuwa wa kusuasua kutokana na sababu mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwemo athari za ugonjwa wa Covid 19,”alisema na kuongeza.

“Chama kimeielekeza Serikali kuhakikisha inabuni mikakati na mbinu za ukuzaji wa uchumi ili kuhakikisha uchumi nchini unakua kwa wastani angalau asilimia nane kwa mwaka, ikilinganishwa na sasa ambao ukuaji ni asilimia 4.8,”alisema.

Aidha alisema ili kuwa na uchumi tulivu, Chama kimeielekeza serikali kuhakikisha kwamba, mfumuko wa bei unadhibitiwa, usizidi tarakimu moja.

“ Udhibiti huu wa mfumuko wa bei utasaidia kukuza biashara za nje, hivyo kutupatia na kuongeza fedha za kigeni nchini na Fedha za kigeni husaidia kununua mafuta (petroli, dizeli) malighafi za viwanda, vipuri, na bidhaa mbalimbali ambazo hatuzalishi nchini ama hazitoshelezi,”alisema.

Shaka alisema ili kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje ambayo mara nyingi imekuwa haiaminiki na hailetwi kwa wakati ili kukamilisha utekelezaji wa bajeti, Chama kimeielekeza Serikali kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kutekeleza dhana na sera ya kujitegemea, hivyo ni lazima serikali ihakikishe inaibua vyanzo vipya vya mapato vya ndani,inaongeza idadi ya walipa kodi ,inakusanya kodi kwa mifumo ya kielektroniki kuziba mianya ya udanganyifu na upotevu wa mapato ya serikali na Uhimilivu wa Deni la Taifa.

Alisema Chama kimeielekeza Serikali kuwa, Deni la Taifa linapaswa kuendelea kuwa himilivu na endapo nchi italazimika kukopa, mikopo hiyo iwe ni yenye tija kwa taifa na isiyoathiri uhimilivu wa deni.

Maelekezo mengine ni serikali kuhakikisha inaimarisha mifuko ya utoaji wa mikopo kwa wananchi,uwezo wa kifedha wa mifuko utawezesha wadau wengi nchini kukopa na kuendeleza shughuli zao kiuchumi, ikiwemo Viwanda, Nishati na Kilimo na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi na pato la mtu mmoja.

Serikali imetakiwa pia kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa katika bajeti kwa kila wizara, zinapelekwa zote na kwa wakati ili kutokwamisha mipango ya maendeleo iliyowekwa.

Join our Newsletter