Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 29Article 554221

Siasa of Sunday, 29 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM kuishitaki TBA kwa Samia

CCM kuishitaki TBA kwa Samia CCM kuishitaki TBA kwa Samia

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa wa Singida kinakusudia kwenda kumuona Mwenyekiti wa CCM wa Taifa, Rais Samia Suluhu ili kumuomba awaondoe Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika shughuli za ujenzi wa majengo mkoani humo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo.

Azimio juu ya uamuzi huo lilitolewa juzi katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho kilichofanyika mjini hapa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Juni 2021.

Taarifa hiyo ilisomwa mbele ya kamati hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Binilith Mahenge.

"Kama kuna chombo kinachotukwamisha katika ujenzi wa majengo ya serikali, basi ni TBA. Hawafanyi kazi kwa wakati na kwa ufanisi unaotakiwa,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama, James Mkwega.

Taasisi hiyo iliyopewa zabuni ya kujenga, kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu katika ujenzi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mkalama na Ikungi kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Juni 2018, inashutumiwa kushindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi amekuwa akitumia ofisi za Shule ya Sekondari Ikungi kwa kipindi chote huku Mkuu wa Wilaya ya Mkalama akifanyia kazi zake kwenye jengo la halmashauri, mazingira yanayotajwa kuwa yanawanyima nafasi ya kufanya kazi kwa uhuru.

Baada ya majadiliano, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Kilimba, alisema yupo tayari kwenda kwa Rais kufikisha suala hilo lipatiwe ufumbuzi mapema.

Alisema atapendekeza kwa Rais Samia TBA ibaki na jukumu lake la msingi la kuanzishwa kwake na si kuwapa zabuni za ujenzi wa majengo.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Singida, Robert Laurent, alisema kusuasua kwa utekelezaji wa ujenzi wa ofisi hizo za wakuu wa mikoa kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na changamoto za miradi yenyewe ikiwemo sababu za kitaalamu na ucheleweshaji wa fedha za miradi tajwa kutoka wizarani.

"Kutokana na ucheleweshwaji huo, kumekuwa na mapitio ya mara kwa mara ya mikataba hali inayosababisha muda wa kumaliza kazi kusogezwa mbele kila wakati.”

“Mapitio ya hivi karibuni yanatutaka kumaliza kazi hizo zote ifikapo Novemba mwaka huu. Kimsingi, tatizo halipo upande wetu," alisema Laurent.