Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558478

Siasa of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

CCM kujadili utendaji wa Wizara ya Afya

Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi(CCM),Taifa Shaka Hamdu Shaka,amesema chama hicho hakiridhishwi na utendaji wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto,katika kusimamia na kutekeleza maagizo na ilani ya chama hicho .

Amesema viongozi wa wizara hiyo wamekuwa na maneno mengi badala ya kuwa watendaji na CCM haiwezi kukubaliana na hali hiyo na kuwataka wapunguze urasimu katika utendaji wao.

Shaka alitoa kauli hiyo mkoani Mtwara,alipofanya ziara ya kukagua maandalizi ya kuanza kazi kwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyojengwa katika eneo la Mitengo Mkoani humo.

Amesema licha ya shirika la Nyumba(NHC),kufanya kazi nzuri ya ujenzi wa jengo hilo na kukamilika kwa asilimia 97,kwa upande wa jengo na asilimia 98 kwa upande wa miundombinu ya ndani na nje,ni wazi hospitali hiyo haitoweza kuanza kazi Oktoba kama alivyoelezwa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, wakati alipoweka jiwe la mSingi Julai Mwaka huu.

“Alipokuja hapa Makamu wa Rais Dk Mpango, wizara ya Afya iliahidi hospitali hii ingekuwa tayari kuanza kazi Oktoba mwaka huu, lakini kwa dalili ninazoziona jambo hilo haliwezekani,na hii yote inasabibishwa na wizara kuwa na maneno mengi kuliko vitendo nawasihi wabadilike chama hakiwezi kuwavumilia”alisema Shaka.

Amesema kazi kubwa ya chama hicho ni kuahidi na kutekeleza maazimio ya chama na ilani kazi aliyoeleza inasimamiwa kwa ufanisi na Mwenyekiti wa chama Samia Suluhu Hassan,ambaye pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa matarajio ya chama hicho ni hospitali ya Rufaa kanda ya kusini kuanza kazi kwa wakati kwa ajili ya kuwapunguzia wananchi wa mikoa ya Mtwara,Ruvuma na Lindi gharama ya kwenda mbali kufuata huduma za kibingwa.

Katika ziara hiyo Shaka, mbali na kueleza kutokuridhishwa na utendaji wa wizara ya Afya, aliwaagiza wasimamie ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kupunguza majukumu kwenye hospitali ya kanda ya kusini pamoja na hospitali ya Rufaa ya mkoa huo.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga,amesema, Rais Samia ameshatekeleza wajibu wake wa kuongeza fedha za kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo na kwamba panahitajika msukumo wa ziada kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana kwa ajili ya kuanza kutumika kwa hospitali hiyo

“Naibu waziri wa Afya alipokuja hapa kwenye ziara ya Makamu wa Rais,alisema tutaanza kutumia hospitali hii ifikapo Oktoba, alikini mpaka wakati huu hakuna kinachoendelea nadhani kunahitajika msukumo wa ziada katika jambo hili”amesema Mtenga

Awali Meneja wa Shirika la Nyumba(NHC), Mkoa wa Mtwara, ambao ni wasimamizi wa ujenzi wa Hospitali hiyo ya Kanda ya Kusini, Mhandisi Angelina Magaza,alisema wanatarajia kukabidhi Jengo hilo la hospitali Septemba 29 mwaka huu baada ya kukamilika kwa kila hatua ya Ujenzi.

Amesema kwa sasa wanawasubiria wakala wa usalama pahala pa Kazi(OSHA kwa ajili ya kuhakiki, ujenzi wa ngazi huku hatua za mwisho mwisho za ujenzi zikiendelea.

Ameeleza mpaka sasa wameshatumia kiasi cha Shilingi bilioni 14.128 kati ya bilioni 15.8 zilizotarajiwa kutumika mpaka mwisho wa mradi.