Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 10Article 546283

Siasa of Saturday, 10 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM yakerwa utekelezaji miradi ya maendeleo Rukwa

CCM yakerwa utekelezaji miradi ya maendeleo Rukwa CCM yakerwa utekelezaji miradi ya maendeleo Rukwa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Rukwa na kumuagiza mkuu wa mkoa huo, Joseph Mkirikiti kuunda kikosi kazi cha kukagua na kufanya tathmini ya miradi hiyo ili kujua ikiwa utekelezaji wake unakidhi thamani ya fedha zilizotumika.

Kutokana na hilo, kimeahidi kuwaita Dodoma mawaziri wanaohusika na sekta za afya, maji, ardhi na Tamisemi ili kujiridhisha juu ya mipango yao na kujua mkwamo ama urasimu unatokea katika eneo gani na kusababisha huduma kusuasua.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema hayo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo aliyoambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichofanyika ukumbi wa mikutano katika Manispaa ya Sumbawanga.

Viongozi hao wakuu wa CCM wamebainisha kutoridhishwa na miradi walioitembelea hasa katika sekta ya afya ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya dawa, wataalamu, huduma duni kwa wazee pamoja na maeneo mengine kuwa na utekelezaji wa miradi isiyoendana na thamani ya fedha iliyotumika.

“Naagiza na kukuelekeza mkuu wa mkoa uunde timu ya wataalamu kwa ajili ya kukagua na kufanya tathmini ya miradi yote inayotekelezwa mkoani kwako ili kujua hali halisi ya kinachoendelea hususani kwenye eneo la thamani ya fedha zilizotumika…hapa mambo hayaendi vizuri kabisa,” alisema Chongolo na kuongeza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ndiyo inayoiongoza serikali kwa miaka hiyo mitano.

Chongolo alisema CCM haiko tayari kulea viongozi na watendaji wazembe wanaoonekana kushindwa kutatua kero za wananchi na kuimarisha ustawi wao, hivyo ndani ya siku 14 atahitaji kupata ripoti ya utekelezaji wa maelekezo hayo na hatua kali zichukuliwe itakapobainika kuna ubadhirifu ama uzembe unaokwamisha ufanisi wa miradi hiyo.

“Nahimiza watendaji wa serikali kuwa waadilifu kwa kuheshimu fedha za umma. Hakikisheni fedha zinazoletwa au kutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatafsirika kwa wananchi kwa kuwaletea unafuu na kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi kwao,” alisema Chongolo.

Aidha, alisema akirejea Makao Makuu Dodoma atawaita mawaziri wanaohusika na sekta za afya maji, ardhi na Tamisemi ili kujiridhisha juu ya mipango yao na kujua mkwamo ama urasimu unatokea katika eneo gani na kusababisha huduma kusuasua na kuwa sio za kiwango na ufanisi kwa wananchi.

Alisema kila kiongozi na mtendaji katika chama na serikali ana wajibu wa kutimiza wajibu wake kwa kuhakikisha upatikanaji wa tija huduma za kijamii unakuwepo kama anavyosisitiza Rais Samia Suluhu Hassan wakati wote.

Akiwa mjini hapa juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Shaka Hamdu Shaka alisema CCM haitaacha kutetea maslahi ya umma, kupigania maendeleo ya kisekta au kutofuatilia ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Alisema kazi ya CCM tangu enzi za TANU na ASP ni kushughulika na maisha ya watu, shida, kero zao, lakini pia kutazama kwa kina iwapo mikakati ya kimaendeleo iliyobuniwa kisera katika maeneo husika inafanyiwa utekelezaji.

Shaka alisema kazi kubwa ya chama hicho ni kutazama iwapo mipango na mikakati ya kisera inabeba uhalisia wa utekelezaji katika kutoa majawabu ya kero za wananchi na kuharakisha maendeleo.

“Lengo la wenzetu (upinzani) ni kutaka kutuondoa kwenye reli ya utelelezaji wa majukumu ya msingi na ya kisera ambayo hata wao wanajua tuliyoyaahidi kwa wananchi, hatutagombana nao wao waendelee kupiga mayowe, sisi tuendeleze ajenda yetu ya kuwatumikia wananchi kwa kuangalia maisha ya watu kwa kutatua shida, kero na changamoto zinazokwamisha maendeleo yao na nchi kwa ujumla,” alisema.

Shaka alisema CCM ni chama makini na hadi sasa hakuna vyama vya siasa makini na mbadala wa chama hicho.