Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 13Article 546814

Siasa of Tuesday, 13 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CCM yasitisha faini za ujauzito Mbeya

CCM yasitisha faini za ujauzito Mbeya CCM yasitisha faini za ujauzito Mbeya

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha faini wanazotozwa wazazi wa watoto wanaopewa ujauzito na watuhumiwa wa vitendo hivyo wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alitangaza uamuzi huo jana wakati akiwa katika mkutano wa Shina 3 Kata ya Kandete, Kijiji cha Mwela Busekelo mkoani humo.

Shaka alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk Vincent Anney asitishe utekelezaji wa uamuzi wa bodi za shule na fedha zote zilizokusanywa kama faini zirejeshwe kwa kwa waliowapa ujauzito wanafunzi na waliopewa ujauzito kutoka shule za sekondari na msingi.

“Hatuwezi kukomesha vitendo vya kuwapa mimba watoto wetu wa kike kwa kuendelea kutozana faini kwa wazazi wote, yaani mtu mwanaye anapewa mimba na pesa anatozwa (245,000) na mifuko 10 ya saruji pamoja na mtenda kosa hilo halafu wote wanarejea kwenye jamii,” alisema Shaka.

Shaka alisema jambo hilo ni kinyume na sheria ya elimu na haiwezekani waliopewa dhamana ya kuisimamia na kutafsiri sheria wabadili maudhui na kutasiri wanavyotaka.

“Maelekezo ya chama, mkuu wa wilaya sitisha utekelezaji wa uamuzi huu kwa shule zote, na fedha zote zilizokusanywa zirejeshwe kwa wahusika na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zichukuliwe,” alisema.

Shaka alisema CCM iinasikitishwa na ongezeko la matatizo ya ujauzito na utoro yaliokithiri kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Rungwe.

Alisema ni ajabu katika halmashauri hiyo wamejiwekea utaratibu wa kuwapiga faini wazazi ambao watoto wao ni watoro au wamepata ujauzito na akasema CCM haitakubali kuona baadhi ya watumishi, watendaji na viongozi wanawagombanisha na wananchi.

“Niwaombe na nitoe raia kwa mawaziri, naibu mawaziri na watendaji wote waliaminiwa na Rais Samia kumsaidia wanapokuja ziara mikoani washuke hadi vijijni kusikiliza wananchi kama anavyofanya Waziri Mkuu Majaliwa.

“Huku kuna shida kubwa wasiridhike na ripoti za mapambio wanazopatiwa, washuke waje waone uhalisi itawasaidia sana kuwatathmini wasaidizi wao wa ngazi za chini kama wanakidhi haja ya mbio za kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Shaka.