Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 30Article 554347

Siasa of Monday, 30 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHADEMA, UDP, UMD kuhakikiwa wiki hii

CHADEMA, UDP, UMD kuhakikiwa wiki hii CHADEMA, UDP, UMD kuhakikiwa wiki hii

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa leo inaanza kuhakiki vyama vya siasa na itaanza vyenye ofisi Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa barua na ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kusainiwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, vyama vitakavyofungua uhakiki huo leo ni AAFP kuanzia saa 2:30 asubuhi na NRA saa 6:30 mchana.

Ratiba hiyo pia inaonesha siku ya kesho, uhakiki utaendelea kwa chama cha UDP na NLD, vikifuatiwa na vyama vya UMD na ADC siku ya Jumatano Septemba Mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Septemba 2, mwaka huu, siku ya Alhamisi, vyama vya CCK na Demokrasia Makini vitafanyiwa uhakiki.

Siku ya Ijumaa itakuwa zamu ya vyama vya Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na UPDP.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uhakiki huo utaendelea hadi wiki ijayo Septemba 6 kwa vyama vya NCCRMageuzi na na CHAUMA kuanzia saa 2:30 asubuhi na saa 6:30 mchana.

Vyama vingine vitakavyohakikiwa wiki hiyo ni ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Tanzania Labour (TLP), SAU, ADA Tadea na DP.

Ratiba hiyo inaonesha uhakiki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utafanyika makao makuu ya chama hicho mkoani Dodoma siku ya Ijumaa Septemba 10, mwaka huu.

Aidha, baada ya uhakiki katika ofisi za vyama Dar es Salaam na Dodoma, uhakiki huo utahamia ofisi za Zanzibar kuanzia Septemba 13, mwaka huu kwa kuhakiki vyama vya AAFP na NRA.

Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kila chama chenye usajili kamili kinatakiwa kuwa na ofisi pande zote mbili za Muungano.

Uhakiki wa vyama vya siasa ni takwa la kisheria kuhakikisha vyama 19 vyenye usajili kamili vinatekeleza masharti ya usajili kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.

Mwaka jana, uhakiki wa vyama hivyo ulifanyika Machi 12 kwa muda wa siku 10, ambapo mambo yaliyoangaliwa ni pamoja na chama kinapaswa kuonesha hati ya umiliki wa jengo la ofisi au kama kinapanga kioneshe makubaliano ya maandishi.

Mahitaji mengine kwenye ofisi ni bendera, bango lenye jina la chama na alama kuepusha uwezekano wa kujibanza eneo lolote na kusema ni ofisi.

Mambo yatakayozingatiwa ni ofisi inatakiwa kuwa na samani, ifikike kirahisi, cheti cha usajili na sera za chama zinatakiwa kuonekana wazi.

Uhakiki pia utaangalia suala la viongozi wa kitaifa, mathalani kama muda wa viongozi wa kukaa madarakani umeisha na utaelekeza uchaguzi ufanyike endapo muda wao umeisha.

Orodha ya mali za vyama ni jambo lingine ambalo uhakiki utazingatia.

Kwa vyama vyenye ruzuku, taarifa ya fedha lazima itofautishe mapato na matumizi mengine na fedha za ruzuku ni lazima ziwe na akaunti yake na taarifa zinapaswa ziwe mbili.

Uhakiki ni utekelezaji wa kawaida wa majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Uhakiki hufanyika kila mwaka isipokuwa mwaka juzi 2019 kulipokuwa na mchakato wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa.