Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 20Article 552571

Siasa of Friday, 20 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHADEMA yahimiza wananchi kuchanjwa dhidi ya Corona

CHADEMA yahimiza wananchi kuchanjwa dhidi ya corona CHADEMA yahimiza wananchi kuchanjwa dhidi ya corona

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewataka Watanzania kuchangamkia chanjo ya Covid-19, kwa kuwa serikali imejiridhisha ubora na usalama wa chanjo hiyo .

Aidha, kimesema chanjo ni jambo la kisayansi na sayansi huwa haiongopi. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hatua ya serikali kukubali kuingiza chanjo ni hatua muhimu kwa sababu ni chanjo iliyozingatia taratibu zote za kisayansi na kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema chama hicho kinashauri Watanzania kwa pamoja na bila woga kwenda kupata chanjo hiyo kwa kuwa ugonjwa wa Covid-19 ni hatari na unaua na kuwaasa waachane na imani potofu zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii.

“Kila kukicha wazee wetu wanaondoka, wanataaluma mbalimbali pia wanaondoka yaani ni msiba baada ya msiba. Corona ipo na ni hatari hivyo, tuna wajibu wa kupiga vita ugonjwa huu kisayansi na kwa kufuata taratibu za kisayansi,” alisema.

Aliongeza kuwa asilimia kubwa ya watu wanaopinga chanjo ya Covid-19 sio wanasayansi, hawana ujuzi wowote kuhusu sayansi na wala hawakuwahi kufanya tafiti zozote za kisayansi katika maisha yao hivyo hata kauli zao ni batili.

Mrema alisisitiza kuwa Tanzania inapokea chanjo nyingi na hazijawahi kuleta madhara. “Tunawahimiza wanachama wa Chadema na Watanzania kwa ujumla popote walipo waende wapate chanjo ili waweze kujikinga na virusi vya corona kwani chanjo inaupa mwili kinga ili kuweza kupambana na virusi endapo mtu atapata maambukizi,” aliongeza Mrema.