Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558475

Habari Kuu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

COVID-19 yasababisha Watanzania zaidi ya 700 kukosa mafunzo India

Waziri wa Elimu, Prof. Ndalichako Waziri wa Elimu, Prof. Ndalichako

SERIKALI imesema mlipuko wa corona umesababisha wanufaika 721 wa Mpango wa Mafunzo Ushirikiano wa Kiufundi na Kiuchumi wa Serikali ya India (ITEC) kushindwa kwenda kwa ajili ya mafunzo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, aliyasema hayo juzi jioni wakati Tanzania na India zikisherehekea ushirikiano huo ambao ulianza mwaka 1972 na kuwezesha Watanzania kwenda India kupata mafunzo mbalimbali.

Prof. Ndalichako alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 na 2019/20 jumla ya nafasi 721 zilitolewa lakini kutokana na mlipuko wa corona, wengi wao hawakwenda mafunzoni.

"Wanufaika ni watumishi katika taasisi za kawaida na pia hutoa nafasi kwa majeshi yetu kushiriki pamoja na watu wanaohusika na masuala ya sheria, wapo Watanzania wengi wanaofanya mafunzo haya India ambao ni takribani 3, 000,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali ya India imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo zinafurahia uhusiano mkubwa ambao ulianzishwa na waasisi wa mataifa hayo.

“Tanzania kupitia programu ya ushirikiano katika masuala ya teknolojia na uchumi tumepeleka wanafunzi wengi India kusoma, tulianza mwaka 1972 na wanafunzi 24 na idadi imekuwa ikiongezeka hadi kufikia mwaka 2017/18 jumla ya nafasi 474 zilitolewa kwa Tanzania,” alisema.

Waziri huyo alisema nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala mengi kwa kuhakikisha wanajenga nguvu kazi wenye weledi uliosheheni ujuzi na maarifa unaohitajika katika dunia ya sasa.

Pia alisema nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala ya teknolojia katika uanzishaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.

Alisema kupitia ushirikiano kati ya nchi hizo, wameanzisha mafunzo ya hali ya juu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Taasisi ya Nelson Mandela, Arusha na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam ambapo India imewezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa zikiwamo kompyuta.

Pia alisema wamepeleka walimu India kusoma ili kuimarisha ujuzi na maarifa katika fani za TEHAMA na wapo ambao wamepata mafunzo katika ngazi ya Stashahada ya Juu (Post Graduate Diploma).

Balozi wa India nchini, Binaya Pradhan, alisema kila mwaka wamekuwa wakisherehekea uhusiano huo ambao unawaleta pamoja wanufaika na kueleza uzoefu wao waliopata India.

Alisema programu ya ITEC ilianza Septemba 15, 1964 na imekuwa muhimu kwa nchi yao kutoa msaada wa kiufundi, uhamishaji wa teknolojia na kujenga uwezo kwa nchi washirika.

“Kwa Tanzania programu hii ilianza mwaka 1972, ilianza na wanufaika 24 na kila mwaka wameongezeka hadi nafasi 500. Zaidi ya raia 4,500 wakiwamo maofisa wapatao 300 wa jeshi nao wananufaika na mpango huu,” alisema.

Mnufaika wa programu hiyo, Elibahati Kimaro kutoka Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, alisema alikwenda India mwaka 2019 kusoma masuala ya taka ngumu za mijini na baada ya kurudi ameanzisha uzalishaji wa mbolea kwa kutumia mabaki mbalimbali ya shambani.