Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540448

xxxxxxxxxxx of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Chanjo ya Covid-19 kuanza kutolewa Z’bar mwezi ujao  

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema mahujaji wanaotarajiwa kutekeleza ibada ya hijja kwenda Makka, Saudia Arabia mwaka huu watapewa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa covid-19 mwezi ujao.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Wanawake, Nassor Ahmed Mazrui alisema chanjo mbili zimeshathibitishwa rasmi na ndizo zitatumika kwa Waislamu wanaotarajiwa kutekeleza ibada ya hijja. Majina ya chanjo hizo yamepelekwa kwa Rais wa Zanzibar kuidhinishwa.

Alitoa taarifa hiyo jana wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, Rashid Abdalla aliyetaka kufahamu sababu za wananchi wanaokwenda nje kutozwa Sh 180,000 kwa kupata kipimo cha covid-19 na kuitaka serikali kutoa msimamo wa chanjo kwa mahujaji watarajiwa.

Mazrui alisema mchakato wa kuwapatia mahujaji chanjo lengo lake kubwa ni kutekeleza masharti na kukidhi vigezo vilivyotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kwa Waislamu watakaotekeleza ibada hiyo.

Alisema kwa jumla zipo chanjo nne ambazo zimetambuliwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO) na zilizo salama kwa ajili ya kutumika kwa wananchi.

“Mheshimiwa Naibu Spika napenda kuwajulisha wananchi pamoja na mahujaji watarajiwa wanaotegemewa kutekeleza ibada ya hijja Makka Saudi Arabia kwamba wasiwe na wasiwasi...safari ipo na chanjo itapatikana ambapo dawa tutayotumia imepatikana na tumemkabidhi Rais kwa ajili ya kuthibitisha,”alisema.

Mwaka jana, Mahujaji wa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, walishindwa kufanya ibada ya hijja kutokana na Serikali ya Saudi Arabia kuzuia kufuatia janga la kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Mazrui alisema baada ya kutolewa kwa chanjo hiyo kwa mahujaji watarajiwa, watu wengine ambao watapewa kipaumbele ni wafanyakazi wa sekta ya afya wanaotoa huduma kwa wagonjwa pamoja na wafanyakazi wa sekta ya utalii ikiwemo Kamisheni ya utalii.

Aidha, alisema watu kuanzia umri wa miaka 50 ambao ni wazee watapatiwa chanjo hiyo kujilinda na maradhi mbalimbali nyemelezi.

Awali, Mazrui aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba jumla ya vyeti feki 200 vilitolewa kwa watu mbalimbali ikiwamo wageni, vinavyoonesha kwamba wamepata chanjo ya ugonjwa wa corona.

Alisema baadhi ya vyeti hivyo vimekataliwa katika nchi walizokwenda na kusababisha malalamiko mengi yanayoonesha wafanyakazi wa sekta ya afya kukosa uaminifu.

“Mheshimiwa Naibu Spika napenda kuliarifu Baraza la Wawakilishi kwamba tumelazimika kukifunga kituo cha kupima corona kilichopo Nungwi baada ya kubaini wafanyakazi wake kufanya udanganyifu mkubwa,”alisema.

Join our Newsletter