Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 21Article 543649

Habari za Mikoani of Monday, 21 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Chanzo watoto kukimbilia mitaani chatajwa

Chanzo watoto kukimbilia mitaani chatajwa Chanzo watoto kukimbilia mitaani chatajwa

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa WLAC, Theodosia Muhulo, wakati wa tamasha la kutoa elimu na kuelimisha watoto kutambua na kuripoti vitendo vya ukatili lililoandaliwa na kituo hicho juzi ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika Juni 16, kila mwaka.

Kongamano hilo lilijumuisha shule za msingi 10 kutoka katika wilaya za Temeke na Kinondoni na liliambatana na mashindano ya uchoraji na kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi.

Akizungumza katika tamasha hilo, Muhulo alisema wapo pia baadhi ya wazazi ambao wanashindwa kuwapatia mahitaji ya msingi watoto hao licha ya kwamba wanaishi nao nyumbani.

“Hali ya umaskini bado ni kubwa nchini, baadhi ya wanaume wanatelekeza watoto wao na kuacha wanawake wakilea peke yao na wengi wanaotelekezwa hawana uwezo wa kumudu mahitaji muhimu ya watoto,” alisema Muhulo.

“Hali hii inachangia baadhi ya watoto kuacha shule na wengine kwenda kuolewa au kuanza ajira kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu. Pia wapo wanaokimbilia mitaani kuombaomba na wengine kujiunga na vikundi hatarishi.”

Kwa upande wake, Leah Mbunda, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alisema wanapokea malalamiko mengi katika dawati lao yanayohusu wanaume kutelekeza watoto wao.

“Na hapa matukio mengi ya wanaume kutelekeza watoto wao tunayoyapokea ni hasa wazazi wanapotengana, kuvunjika kwa ndoa na imekuwa sababu kubwa sana kuwaharibu watoto hawa,” alisema Mbunda.

“Wakati mwingine kesi tunazozipokea unakuta ndoa inapovunjika, baba anaenda kuanzisha familia nyingine au mama naye anaenda kuolewa, kwa hiyo watoto wanaenda kuishi na bibi ambaye hana uwezo wa kuwalea.”

“Kwa hiyo watoto wanatawanyika kwenda popote na inapotokea wakaangukia katika mikono isiyo salama ndiyo wengi wao wanaharibikiwa na wengine kuingia kwenye kuvuta bangi na mambo mengine mabaya.”

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kinondoni, Agnes Mbusa, alisema wazazi bado wanachangia watoto wao kufanyiwa ukatili kwa sababu wanakubaliana na watuhumiwa kumalizana kimya kimya.

“Na ndiyo maana inakuwa ni vigumu kukomesha hili tatizo kwa sababu hata tunapolifikisha kwenye vyombo vya sheria tunakosa ushahidi,” alisema Mbusa.