Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 11Article 546448

Habari Kuu of Sunday, 11 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Chuo Kikuu Mzumbe chabuni mradi wa ufuatiliaji maji

Chuo Kikuu Mzumbe chabuni mradi wa ufuatiliaji maji Chuo Kikuu Mzumbe chabuni mradi wa ufuatiliaji maji

CHUO Kikuu cha Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Antwerp cha Ubelgiji, kimebuni na kuendesha mradi wa Fuatilia Maji, unaolenga kuangalia maeneo matatu ambayo ni upatikanaji wa maji, vyanzo na ubora wa matumizi yake kwa binadamu vijijini.

Mpaka sasa mradi huo umevifikia vijiji 11 katika wilaya ya Mvomero na Halmashauri ya Morogoro Vijijini, huku malengo yakiwa kufikia mikoa yote nchini na kuisaidia serikali ngazi za halmashauri kuchukua hatua za kunusuru afya za watu na kulinda vyanzo vya maji.

Akizungumza na HabariLEO katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, kampasi ya Dar es Salaam ambaye pia ni mratibu wa mradi huo, Dk Mursali Milanzi, alisema umelenga kuboresha huduma za maji hasa maeneo ya vijijini.

“Tunatumia teknolojia za kisasa za mtandao kama simu za mkononi au tablets kukusanya taarifa. Mradi huu unawashirikisha wanafunzi na tunawajengea uwezo wananchi wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika za vijiji au wilaya kuhusu ubora au tatizo katika chanzo cha maji,” alisema Dk Milanzi.

Alisema wanapima maji katika vyanzo kwa kutumia kidonge maalum cha kupima maji na maji yakigeuka rangi ya udongo na kubaki na rangi hiyo kwa saa 24 ni salama, lakini Yakigeuka rangi ya buluu, hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Alisema hatua wanazochukua wakikuta katika chanzo cha maji kuna tatizo, husimika bendera iliyobeba rangi inayomaanisha maji ni salama au si salama.

Alisema wametengeneza bendera ya rangi nyekundu (maji si salama hayafai kwa matumizi), rangi ya chungwa (maji ni masafi lakini si salama) na rangi ya kijani inayomaanisha maji ni safi na salama kwa matumizi.

Alisema mradi huo ni wa miaka mitano ulioanza mwaka 2017 hadi 2022.

Mwanafunzi wa chuo hicho anayehusika katika mradi huo akichukua Shahada ya Uchumi, Eliya Lushiku aliiomba serikali iusambaze mradi huo nchi nzima ili kusaidia kuondoa haraka changamoto za maji zinazowakumba wananchi hasa vijijini.