Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 15Article 551599

Habari Kuu of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Corona ilivyozua balaa kwenye ajira DSM

Corona ilivyozua balaa ajira Dar Corona ilivyozua balaa ajira Dar

JANGA la corona limesababisha jumla ya wafanyakazi 1,075 wa Mkoa wa Dar es Salaam kuingia katika migogoro na waajiri wao katika kipindi cha robo mwaka tangu ugonjwa huo kuripotiwa nchini.

Ofisa Mfawidhi Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Kanda ya Dar es Salaam, Nahshon Mpula, alibainisha hayo jana alipomwakilisha Mkurugenzi Mkuu wake katika kikao cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kilichoitishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi.

“Huwa tunaripoti mara nne kwa mwaka. Kwa hiyo, kwa robo mwaka hii ambayo imehusisha vipindi vya corona, migogoro 1,075 tuliipokea, jambo ambalo sio la kawaida, hapa tunamaanisha ajira zenye idadi hiyo ziliathirika,” Mpula alifafanua.

Alisema katika utatuzi wa migogoro iliyopokewa, asilimia 86 ilimalizwa kwa kusikilizwa kwa wakati na kwa mkakati maalum.

“Tulichokifanya kwa maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu wa CMA, ni kutoa taarifa na kusababisha kiundwe kikosi kazi kwa kuwachukua wasuluhishi na waamuzi kutoka mikoa mbalimbali waishambulie Dar es Salaam kwa sababu Dar es Salaam ilikuwa ni moja ya maeneo yaliyoathirika sana," alisema.

Ofisa alisema mtu anapochelewesha kufungua mgogoro wa kikazi, anahatarisha kupoteza haki zake za msingi, hivyo akasisitiza yeyote aliyeachishwa kazi, anatakiwa kufungua shauri ndani ya siku 30.

“Mgogoro mwingine wa haki kwa mujibu wa sheria za kazi nchini, mbali na ule wa kuachishwa kazi, anatakiwa aulete ndani ya siku 60 kwa ajili ya utekelezaji,” alisema.

Ofisa huyo alisema katika andiko lake la mwaka juzi, ongezeko la migogoro ya kikazi ni kubwa zaidi, hivyo kuathiri kwa namna moja kukua kwa uchumi.

Alisema sheria imeweka masharti migogoro imalizike ndani ya siku 30 lakini wao wamejiwekea ndani ya siku 21 katika hatua ya usuluhishi na chini ya miezi mitatu katika hatua za uamuzi kwa kuwa wanatambua vijana wana mchango mkubwa katika uchumi.

“Kwa kipindi hiki cha karibuni hasa kipindi hiki cha corona, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la migogoro kwa sababu waajiri wengi wamelazimika kupunguza wafanyakazi mahala pa kazi ama kwa kuwaachisha, kuwapeleka likizo bila malipo, hii ni baadhi ya (migogoro) ambayo imekuwa ikiletwa katika tume,” alisema.

Alibainisha inapoonekana migogoro ipo kwa wingi, Mkurugenzi Mkuu wa CMA anaweka mkakati maalum wa kuteua wasuluhishi na waamuzi kwenda kuweka kambi eneo husika ili kuimaliza kwa wakati ndani ya muda mfupi.

Naibu Waziri Katambi alifafanua zaidi kuwa baada ya migogoro kuwasilishwa CMA, hatua ya kwanza huenda katika usuluhishi na ipo inayoishia hatua hiyo.

“Ikitokea usuluhishi umeshindikana, wanakwenda hatua ya pili ya uamuzi kupitia mfumo wa kimahakama, ambapo hukumu ikitoka inakwenda katika utekelezaji, unakaziwa hukumu kwa Msajili Mahakama Kuu,” alisema.

Kuhusu uanzishaji wa Baraza la Vijana, Katambi alisema mchakato wake umeanza na kesho wizara zote zinatarajia kukaa na kwa hatua ya kwanza watafanya mabadiliko ya Sera ya Vijana ya Mwaka 2007 ili kulipata.

Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari katika Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Jumanne Issango, alisema tume hiyo imetengeneza mwongozo wa kutawanya mipira ya kiume na kike (kondomu) ambao unaelekeza Kitengo cha Udhibiti Ubora cha Bohari ya Dawa (MSD) kurahisisha upatikanaji wa mipira hiyo.

“Takwimu zinaonyesha watu 77,000 wanapata maambukizi ya UKIMWI kwa mwaka, asilimia 40 ni vijana na katika asilimia hiyo, asilimia 80 ni vijana wa kike wenye umri wa miaka 15 hadi 24. Kwa hiyo, tumewaweka vijana kama kundi la kipaumbele,” alisema.

Ofisa Kazi Mkuu Kitengo cha Huduma za Ajira (TAESA), Peter Ugata, alisema jumla ya vijana 7,701 wameunganishwa katika ajira mbalimbali na vijana 10,111 wanafanyiwa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi, kote wanalipwa Sh. 150,000 kila mwezi kama gharama za kuwasaidia.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, alisema utafiti mwaka 2019 unaonyesha kundi kubwa linaloathirika na ajali na vifo sehemu za kazi ni vijana.

“Utafiti ulihusisha mikoa saba, ajali zilikuwa 1230, ajali 841 zilikuwa sekta ya uzalishaji na walikuwa vijana kati ya umri wa miaka 18 mpaka 35,” alibainisha.