Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572680

Habari za Mikoani of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

DC apiga 'Stop' wanafunzi kukalia matofali

DC Tanganyika apiga ‘stop’ wanafunzi kukalia matofali darasani DC Tanganyika apiga ‘stop’ wanafunzi kukalia matofali darasani

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika (DC), Onesmo Buswelu amepiga marufuku wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtapenda kukaa kwenye matofali wakati wa masomo akidai kuwa hana urafiki na watumishi wazembe wanaosababisha hali hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Mtapenda leo Ijumaa Novemba 19, 2021 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa katika shule hiyo, amesema hajafurahishwa kuona wanafunzi wanakaa kwenye matofali.

“Sijafurahishwa wanafunzi kukaa kwenye matofali, ninawaagiza kamati yenu ikae haraka, madawati yaanze kutengenezwa kesho mkishindwa nitawawajibisha, madarasa haya yakikamilika na madawati yawe tayari” amesema Buswelu akaongeza.

“Wananchi mmefanya kazi kubwa sana mmesomba mchanga, matofali, maji na mawe lakini wapo watumishi ambao kasi yao haiendani na nyie pamoja na Rais, wanafanya uzembe sitakubaliana nao,”amesema.

Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, Neema John amesema hali hiyo ya kukaa kwenye matofali wakati wa masomo inawaathiri kielimu.

“Tunashindwa kuandika vizuri wakati mwingine magoti yanauma kwasababu tunakunja miguu kwa muda mrefu, tunaomba tutengenezewe na madawati,”amesema Neema.

Naye, Dioniz Shigela ambeye ni mkazi wa eneo hilo amesema wameamua kushiriki kikamilifu ili mradi wa ujenzi wa madarasa ukamilike kwa wakati.

“Ukikamilika watoto watasoma vizuri tutapata marais, kuna madarasa matano tu wengine wanakwenda kusoma Sibwesa ni mbali mvua zikinyesha barabara zinaharibika wanapata shida kupita,”amesema Shigela.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Sibwesa, Megamo Megamo amesema wamepokea Sh480 milioni kwaajili ya ujenzi wa shule ya msingi Mtapenda, Magogo na Kamlega.

‘Fedha hizi zimegawiwa Sh160 milioni kila shule ambazo zipo kwenye vitongoji, hapa Mtapenda mradi umefikia hatua ya kufunga lenta wananchi wanashiriki vizuri sana,”amesema Megamo.