Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 15Article 557497

Maoni of Wednesday, 15 September 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

DK STERGOMENA TAX Rais amekupamba kwa heshima mpambe kwa utumishi

DK STERGOMENA TAX  Rais amekupamba kwa heshima mpambe kwa utumishi DK STERGOMENA TAX Rais amekupamba kwa heshima mpambe kwa utumishi

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan aliandika historia nyingine nzito kwa Tanzania katika nyanja ya usawa wa kijinsia katika uongozi.

Ikumbukwe kuwa, Rais Samia anazo historia kubwa kwa Tanzania.

Kwanza, Samia ndiye mwanamke wa kwanza Mtanzania kuwa mgombea mwenza katika chama tawala (Chama Cha Mapinduzi-CCM) na hatimaye kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu Novemba, 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na Mwaka 2020, CCM iliibuka na ushindi uliomfanya kukaa katika wadhifa huo.

Hata hivyo, Machi 19, 2021, Samia aliandika historia nyingine nchini na katika sura ya kimataifa kwa kuwa, Rais wa Kwanza Mwanamke Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu.

Katika kipindi chote alichokuwa madarakani akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania na hata alipochaguliwa na CCM kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Kitaifa wa CCM, utendaji wake uliotukuka umetoa picha halisi hata kwa wabishi kuwa, ‘wanawake wanaweza kuongoza.’

Wachambuzi mbalimbali wanasema kwa kuwa wapo watu wenye mawazo ya kijamaa katika nchi za kibepari huku kukiwa na watu wenye mawazo ya kibepari katika nchi za kijamaa, ndivyo hivyo kwamba kwa kuwa wapo wanaume wengi wanaoshindwa uongozi, ndivyo ilivyo pia kwamba wapo wanawake wengi wanaoweza kuongoza kwa ufanisi.

Ndiyo maana ninasema, Dk Stergomena Tax hana budi kulipamba na kulitunza taji la heshima alilovishwa na Rais Samia kwa kuwa kupitia utumishi bora uliotukuka kwa Watanzania.

Ikumbukwe kuwa, Ijumaa iliyopita Rais Samia alimteua Dk Stergomena kuwa Mbunge.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alimwapisha siku hiyohiyo bungeni Dodoma, zikiwa ni siku chache tangu mwanamke huyo Mtanzania amalize majukumu yake ya kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) alipohudumu kwa miaka minane tangu Agosti, 2013.

Vazi lingine kubwa la heshima ambalo Rais Samia amemvisha Dk Stergomena Tax, ni kumteua na kumwapisha juzi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kushika nafasi iliyoachwa wazi na Elias Kwandikwa aliyefariki dunia Agosti 2, mwaka huu.

Kutokana na uteuzi huo, Stergomena (61) amekuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Wizara ya Ulinzi hapa Tanzania tangu Uhuru na hii ndiyo heshima kubwa ninayoiita taji la heshima alilovalishwa na rais.

Stergomena amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya kuteuliwa kwenda kuwa mtendaji wa SADC yenye makao makuu yake nchini Botswana.

Sambamba na uteuzi wa Dk Stergomena, Rais pia alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kuwarejesha katika baraza January Makamba, Profesa Makame Mbarawa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango chini ya Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2015 hadi 2020, Dk Ashatu Kijaji.

Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa mkoani Dodoma, ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akichukua nafasi ya Dk Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Awali, taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu Ikulu Jumapili, ilisema katika mabadiliko hayo, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, aliteuliwa na kuapishwa juzi kuwa Waziri wa Nishati akichukua nafasi ya Dk Medard Kalemani ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Mbunge wa Mkoa kisiwani Pemba, Profesa Mbarawa amerejea katika Baraza la Mawaziri katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi akishika nafasi aliyokuwa nayo Dk Leonard Chamuriho ambaye pia uteuzi wake ulitenguliwa.

Mbarawa alikuwa Waziri wa Maji mwaka 2018 hadi 2020; aliwahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2016 hadi 2018 pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuanzia 2010 hadi 2015.

Aidha, Rais Samia pia alimteua aliyekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Eliezer Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Profesa Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Ninawapongeza wote walioteuliwa katika uteuzi huu, lakini pia ninawashukuru walioondolewa katika nafasi zao kwa kipindi walichowatumikia Watanzania kwa nafasi hizo. Katika hafla ya kuwaapisha wateule Ikulu Dodoma, Rais Samia alisema mabadiliko hayo ni ya kawaida.

Nitumie fursa hii kuwaambia wote kuwa, heshima aliyowapa Rais Samia wanapaswa kuilinda mithili ya yai kupitia utii, uadilifu, uaminifu na utumishi uliotukuka kwa Watanzania. Kwamba, asiwepo ‘anayetembea usiku kama bundi’ au ‘anayetembea’ wakati wenzake ‘wanakimbia’ kuelekea maendeleo ya taifa.

Kipekee kwa Dk Stergomena ni kukumbuka na kuzingatia kuwa, Rais Samia amempa heshima tatu kwa pamoja, hivyo anapaswa kuzilinda na kuziheshimu.

Hizi ni kwanza, ile heshima tu ya kustaafu SADC ndani ya siku chache tu, akamteua ubunge na ndani ya siku chache nyingine, akamteua kuwa waziri, lakini heshima ya kuwa waziri katika wizara ambayo haijawahi kuongozwa na mwanamke na sasa anakuwa mwasisi. Hiyo ni imani na heshima kubwa.

Ndio maana Rais katika hafla ya kuwaapisha aliamua kuweka bayana na kusema: “Katika mabadiliko haya, nimeamua kuvunja mwiko wa muda mrefu kwamba Wizara ya Ulinzi lazima akae mwanaume kwenye misuli yake, lakini kazi ya waziri kwenye wizara ile si kupiga mizinga wala kubeba bunduki, ni kusimamia sera na utawala wa wizara. Nikaamua dada yetu Stergomena Tax nimpeleke huko.”

Akaongeza: “Nimempeleka huko kwa sababu ya upeo wake mkubwa alioupata akiwa SADC. Kipindi chote tukienda SADC, alikuwa anasimamia vyema mambo yote ya usalama ndani ya jumuiya, na pia alikuwa na upeo mkubwa katika maeneo ya Afrika Mashariki.”

Rais Samia akaweka bayana kuwa, anaamini Dk Stergomena ataisaidia wizara hiyo pia kwa sababu anajua vyema askari wa Tanzania waliopo Msumbiji na DRC na mambo mengine yote, hivyo atamsadia vizuri Mkuu wa Majeshi katika eneo hilo.

Utendaji na utumishi bora uliotukuka wa Dk Stergomena na wenzake, unapaswa kuwa ndio malipo ya heshima aliyowapa Rais Samia kwa kutaka wamsaidie katika uongozi maana wapo Watanzania wengi wenye uwezo wa kuongoza.

Kwa msingi huo, wanapaswa kuzingatia kuwa utii ni bora kuliko sadaka. Wamtii kwa viwango vyote Rais, lakini wasikilize na kutafuta majawabu ya walio chini yao maana Tanzania ni moja ya Watanzania na itajengwa na Watanzania.

Katika kusisitiza kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa manufaa ya taifa, Rais Samia akasisitiza: “Tunapoendelea huko, serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na si maneno makali. Ninaposema matendo makali si kupigana mijeledi, ni kwenda kwa wananchi na kutoa huduma inayotakiwa.”

Ndio maana ninasema, Dk Stergomena na viongozi wengine wateule wa rais wageni na waliokuwapo, Rais Samia amewavisha taji kubwa la heshima, mlipeni shukrani zenu kupitia matarajio na matanamio yake kwa utumishi bora na wenye ufanisi kwa Watanzania na taifa kwa jumla.

Dk Stergomena, soma kwa makini fursa zilizopo katika wizara yako; ‘uzichume na kuzila’ na Watanzania wote wakiwamo watendakazi wizarani kwako.

Jifunze changamoto zilizopo wizarani kwako na kuzitafutia majawabu kupitia hasahasa ‘meza ya majadiliano’ kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyopo ukizingatia kuwa, utii ni bora kuliko sadaka maana Rais amekuvisha taji la heshima, lilinde kupitia utumishi wako kwa umma.