Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 12Article 562702

Habari Kuu of Tuesday, 12 October 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Dar: Mtendaji wa Mtaa Auawa kwa Mapanga Ofisini Kwake

Mauaji Mauaji

Mauaji ya kutisha yametokea eneo la Mbezi Msumi mkoani Dar es Salaam baada ya watu wasiofahamika kudaiwa kuvamia ofisi za Serikali ya Mtaa wa eneo hilo na kisha kumuua Ofisa Mtendaji kwa kumkata na panga.

Tukio hilo la mauaji limetokea jana Oktoba 11, 2021 kati ya saa sita hadi saa saba mchana na inadaiwa ofisa huyo mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Msumi Jijini Dar es salam ameshambuliwa kwa kukatwa na panga shingoni na watu ambao hawafahamiki.

Mmoja wa mashuhuda na mwananchi wa eneo hilo(jina limehifadhiwa) amedai wameshangazwa na tukio hilo la mauaji ambalo limefanywa kwa kiongozi huyo.

Alipoulizwa iwapo watu waliofanya tukio wamefahamika, amejibu hawajafahamika kwani baada ya kutekeleza unyama huo walikimbia na haijulikani ni akina nani na wametoka wapi, ingawa anaamini Jeshi la Polisi linajua namna ya kufuatilia tukio hilo na kuupata ukweli.

"Wananchi tumejawa na taharuki baada ya kutokea tukio hili la mauaji , hatuji nini kimesababisha hadi watu hao kufanya unyama huu kwa kiongozi wa Serikali ya Mtaa,tupo hapa tunasubiri kuona nini kinachoendelea," amesema shuhuda huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhan Kingai amethibitisha kupata taarifa hizo za tukio la mauaji na tayari askari polisi tayari wako eneo la tukio."Tumepata taarifa za tukio hilo,tunafuatilia na baadae tutatoa taaria rasmi kwa vyombo vya habari."