Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 05Article 541129

Diasporian News of Saturday, 5 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dk Mwinyi: Tuko tayari kupokea chanjo za COVID-19

Dk Mwinyi: Tuko tayari kupokea chanjo za COVID-19 Dk Mwinyi: Tuko tayari kupokea chanjo za COVID-19

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali iko tayari kupokea msaada wa chanjo COVID -19 pamoja na misaada mbali mbali ya kitabibu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dk Mwinyi alisema hayo juzi Ikulu, Zanzibar , alipokutana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani, anayefanyia shughuli zake nchini, Tigest Ketsela Mengestu, aliyefika kujitambulisha.

Alisema sekta ya afya nchini ina mahitaji makubwa ili iweze kufanikisha lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisema azma ya WHO kuendelea kusadia Zanzibar katika nyanja mbali mbali, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa afya pamoja na uimarishaji wa miundombinu ni jambo muhimu.

Alisema katika hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwapo Bima ya Afya nchini.

Aidha, alisema ipo haja ya kuimarisha miundo mbinu ya huduma za afya, hususani katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambayo hivi sasa haikidhi mahitaji ya wakati katika utoaji wa huduma kutokana ongezeko la watu pamoja na ufinyu wa nafasi.

Rais Dk. Mwinyi alilishukuru shirika hilo kwa ushirikiano pamoja na misaada mbali mbali inayotoa kwa Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Mengestu, alisema WHO iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala la kuimarisha sekta ya Afya nchini, hususan katika utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa sekta hiyo.

Alisema Shirika hilo linalenga kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kukabiliana na magonjwa mbali mbali kama vile kipindupindu, ukosefu wa lishe, mafua makali pamoja na covid -19.

Aliomba serikali kubainisha aina ya chanjo ya COVID-19 inayohitajika, sambamba na kuhakikisha mchakato wa kuwapatia chanjo Mahujaji wa Zanzibar unakamilika kwa wakati, ikizingatiwa kuwa umebaki muda mfupi kabla ya ibada hiyo.

Wakati huo huo Dk Mwinyi alizungumza na Mwakilishi mkaazi wa ‘UN Women Tanzania’ Hodan Addou, na kumhakikishia kwamba serikali iko makini kuhakikisha wanawake wa Zanzibar wanapata haki zao pamoja na kuondokana na vitendo vyote vya ukandamizaji, ikiwemo udhalilishaji dhidi yao na watoto.

Addou alimpongeza Dk Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika Uongozi, sambamba na juhudi zinazofanyika katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.

Join our Newsletter