Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 20Article 543442

Diasporian News of Sunday, 20 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dk Mwinyi aitaka EAC iende kwa wananchi

Dk Mwinyi aitaka EAC iende kwa wananchi Dk Mwinyi aitaka EAC iende kwa wananchi

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wakati umefika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya kazi kwa karibu na wananchi waweze kutambua umuhimu wa kuwepo jumuiya hiyo.

Alisema hayo jana Ikulu, Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki, uliofika kwa ajili ya kusalimiana naye.

Dk Mwinyi alisema azma ya Jumuiya hiyo kufanya baadhi ya vikao vyake vya Bunge pamoja na Mahakama Zanzibar, itawafanya wananchi wawe na uelewa wa kuwepo kwake na kujenga imani nayo.

Alisema hatua ya ujumbe huo kukutana na viongozi wa sekta binafsi Zanzibar ni jambo jema, hususani katika uimarishaji wa biashara kwa kuzingatia kuwa wadau kutoka sekta binafsi ndio wanaofanya biashara.

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza biashara pamoja na kuondokana na vikwazo mbali mbali vilivyopo .

Rais alisema upo umuhimu wa kutumia ipasavyo bahari kuimarisha uchumi wa Taifa na kubainisha Zanzibar kuwa na sera ya Uchumi wa Bluu.

“Katika uchumi wa bluu kuna sekta kadhaa, ikiwemo utalii, uvuvi, mafuta na gesi, miundombinu ya bandari pamoja na usafirishaji wa baharini, lengo ni kuupa nguvu uchumi huo, pamoja na kuwepo bahari bado haijatumika vilivyo, hivyo ni vyema tukaweka nguvu katika kuimarisha uchumi,” alisema.

Alisema viongozi hao wakiwa wadau wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanapaswa kufikisha ujumbe kwa nchi wanachama kuwa Zanzibar iko tayari kupokea wawekezaji.

Akizungumzia Kamisheni ya Kiswahili, alisema amefurahishwa na juhudi zinazoendelea katika kuimarisha Kamisheni hiyo katika uimarishaji majengo pamoja na upatikanaji wa huduma, hatua itakayosaidia kuiendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda pamoja na Bara zima.

Aidha, alisema wakati umefika wa kuhakikisha ubora wa viwango wa bidhaa zinazozalishwa kutoka miongoni mwa nchi wanachama, zinasajiliwa na kutumika katika nchi zote wanachama wa Jumuiya hiyo.

Alipongeza uwepo wa miradi kadhaa ya pamoja ya maendeleo, ikiwemo ya miundombinu ya barabara katika nchi wanachama na kutumia nafasi hiyo kuishauri Jumuiya kuipatia fursa Zanzibar katika miongoni mwa miradi itakayoanzishwa, ikiwa ni hatua ya kukuza ushirikiano.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Mathuki, alisema hali ndani ya Jumuiya hiyo sasa ni shwari, lengo likiwa ni kuipeleka karibu na wananchi.