Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572665

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Dk Ndumbaro aonya watakaofuja fedha za hifadhi

Dk Ndumbaro aonya watakaofuja fedha za hifadhi Dk Ndumbaro aonya watakaofuja fedha za hifadhi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amewataka watumishi wa hifadhi za Taifa nchini kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya hifadhi ikiwemo barabara na madaraja.

Waziri Ndumbaro ametoa agizo hilo alipokuwa kwenye hifadhi ya Taifa ya Tarangire wilayani Babati mkoani Manyara.

Ameonya matumizi mabaya ya fedha za kuboresha miundombinu ya hifadhi za Taifa na akisema watakaobainika watachukuliwa hatua.

Amesema watakaoshindwa kusimamia fedha hizo za kukarabati miundombinu ya hifadhi za Taifa nchini ni bora wake pembeni na kuwaachia wenye uwezo.

"Watakaofuja fedha hizo ni bora wajiuzulu kwani tutawachukulia hatua kali na Rais Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa atakayegusa fedha hizo ataona rangi yake halisi," amesema Waziri Ndumbaro.

Amesema miundombinu ya hifadhi inapaswa kuimarishwa ili iweze kuvutia watalii wengi zaidi kwenye hifadhi mbalimbali.

Amewataka kushirikiana na viongozi wa Serikali wa wilaya na mikoa inayowazunguka ili kudhibiti maeneo ya ambayo wanyama wanapita (shoroba) yawe ya usalama zaidi.

Naibu kamishna wa uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho ameipongeza Serikali kwa kutoa Sh6 bilioni kwenye hifadhi za eneo hilo.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Ignace Gara amesema licha ya mafanikio waliyonayo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.