Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 10Article 546325

Habari Kuu of Saturday, 10 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dk Shoo wa KKKT mwenyekiti  mpya CCT  

Dk Shoo wa KKKT mwenyekiti  mpya CCT    Dk Shoo wa KKKT mwenyekiti  mpya CCT  

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ,Dk Frederick Shoo amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kipindi cha miaka minne.

Alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa 31 uliofanyika mjini Morogoro tangu Julai 8-9 mwaka huu. Mkutano huo ulifunguliwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan .

Msimamizi wa uchaguzi , Askofu Oscar Mnung'a wa kutoka Kanisa la Anglikana , Dayosisi ya Newala alisema , wapiga kura kwenye uchaguzi huo walikuwa 210.

Nafasi ya Mwenyekiti wa CCT , wagombea walikuwa ni Maaskofu watano na Askofu Shoo alipata kura 63 na kuwashinda wenzake wanne.

Wagombea wengine walikuwa, mtetezi wa nafasi hiyo, Askofu Dk Alinikisya Cheyo wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi ambaye alipata kura 47 .

Wengine na kura zao kwenye mabano ni Askofu Dk Stanley Hotay ( 50) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro , Askofu Dk Mahimbo Mndolwa (29) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga na Askofu Musa Magwesela wa Kanisa la African Inland Tanzania (AICT) , Dayosisi ya Geita aliyepata kura (23).

Msimamizi wa Uchaguzi, Askofu Mnung'a alisema ushindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCT ulikuwa ni aliyeongoza kwa kura nyingi.

Askofu Hotay amekuwa Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti na Askofu Cheyo kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti. Mchungaji Dk Moses Matonya ametetea nafasi yake ya kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya.