Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572941

Habari Kuu of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dk Stergomena awataka vijana kulinda amani ya nchi

stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya nchi na kutoingia kwenye mambo ambayo yanahatarisha usalama.

Alitoa wito huo jana kwenye mkutano wa 56 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wa wanazuoni kabla ya mahafali ya chuo hicho, mjini Dodoma jana.

Alisema vijana wana nafasi kubwa katika kulinda amani ya taifa.

“Ninyi vijana mna nafasi kubwa katika kuhakikisha amani ya taifa letu inadumu, kuna mengi ambayo mmeyaona, kuna mengi ambayo mnashiriki lakini hakikisheni katika yale mnayoshiriki mnayafanya katika njia ambayo inahakikisha ya kwamba mstakabali wa taifa letu unabaki imara na amani inaendelea kutamalaki,” alisema.

Aliwataka pia vijana kutumia vyema mitandao ya jamii na kufanya utafiti na tathimini ya wanayoyaona kwenye mitandao kabla ya kushiriki.

“Kwenye mitandao ya kijamii mnaongea mengi na mnasikia mengi lakini kuna msemo wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akili za kuambiwa changanya na zako.

Ninyi ndio maana mmeletwa kusoma na ndio maana mko kwenye taasisi ambayo pia inafanya tafiti na tathimini. Kwa hiyo kila kitu mnachosikia na kuona kifanyieni tafiti na tathimini kabla hujajiunga katika mambo ambayo hayana faida kwako binafsi na hayana faida kwa nchi yako na hayaleti mandeleo isipokuwa yanenda kuleta taharuki epukeni nayo, ujana una mambo mengi lakini hakikisha ujana wako unakuwa mzuri ambao utahakikisha historia yako inabaki kuwa nzuri maisha yako yote,” alisema.

Aidha, Dk Tax ambaye amehitimu katika chuo hicho miaka 37 iliyopita katika kozi ya usimamizi wa biashara, alisema juhudi katika masomo na kila unachotakiwa kufanya ndio msingi wa mafanikio.

Alisema wakati anahitimu masomo yake chuoni hapo alimaliza akiwa wa pili nafasi ambayo hakuwa anaitegemea kwani aliamini kuwa angekuwa wa kwanza.

“Hiyo ya kuwa nafasi ya pili kwa wanafunzi bora mpaka sasa nikiikumbuka machozi huwa yananitoka maana nilijiamini kuwa ningekuwa wa kwanza,” alisema.

Alisema baadaye alikwenda kujiunga chuo kikuu na kutokana na kufanya vizuri alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 waliochaguliwa kufanya kazi Wizara ya Fedha.

Dk Tax alisema baadaye alipata nafasi ya kwenda kusoma nchini Japan ikiwa na udhamini uliotolewa na Benki ya Dunia na serikali ya Japan na kulikuwa na nafasi 10 dunia nzima.

“Nilikweenda kusoma Shahada ya Uzamili lakini kutokana na kufanya vizuri, chuo kikanipa nafasi ya kusoma PHD,” alisema.

Alisema baada ya kurejea nchini amefanya kazi katika mashirika na taasisi mbalimbali zikiwamo za utafiti na baadaye kuwa Katibu Mkuu Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na sasa Waziri wa Ulinzi na kuwa yote hayo yametokana na juhudi katika nafasi na fursa anazopata.