Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 11Article 546460

Habari Kuu of Sunday, 11 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dk Tulia avitaka vyombo vya habari kutoa taarifa hali ya hewa

Dk Tulia Ackson Dk Tulia Ackson

NAIBU Spika, Dk Tulia Ackson amevitaka vyombo vya habari kutenga muda wa kutosha kurusha taarifa za hali ya hewa mara kwa mara ili kusaidia wananchi kuzipata kwa wakati na kuzitumia katika shughuli zao za kila siku.

Amesema kutokana na muda wa habari za hali ya hewa unaotolewa kuwa mfupi, taarifa hizo kutolewa kwa ujumla na kwa ufupi, kitu ambacho hakileti ufanisi mkubwa.

“Nitoe wito kwa vyombo vya habari kuangalia namna ambavyo watakuwa wanazitumia taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kuzitoa mara kwa mara ili kutusaidia wananchi kujiandaa na kufanya maamuzi sahihi katika mipango yetu, tuangalie kama vyombo vingine vya habari vya mataifa ya nje, ukifungua kila wakati unaangalia hali ya hewa,” alisema Dk Tulia alipotembelea Makao Makuu ya TMA juzi.

Alito mwito kwa wananchi kuitembelea TMA ili kujifunza masuala mbalimbali ikiwamo namna taarifa za hali ya hewa zinavyochakatwa kitaalamu hadi kumfikia mtumiaji.