Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 25Article 565567

Habari Kuu of Monday, 25 October 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Dkt.Mpango akutana na Pope Theodoros II Ikulu DSM

Dkt. Philip Mpango akiwa na Beatitude Theodoros II Ikulu ya Dar es Salaam Dkt. Philip Mpango akiwa na Beatitude Theodoros II Ikulu ya Dar es Salaam

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango jana Oktoba 24,2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Baba Mtakatifu Beatitude Theodoros II (The Pope and Patriarch of Alexandria and all Africa) Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Greek Orthodox Ikulu Jijini Dar es salaam.

Dkt. Mpango amesema Tanzania imefurahishwa na ujio wa Baba Mtakatifu huyo na kumuomba kuendelea kuiweka nchi ya Tanzania katika maombi yake ya kila siku.

Amesema kuwa tangu kupata uhuru Tanzania imekua kitovu cha Amani na kuendelea kuheshimu umuhimu wa dini zote kupitia ibara ya 19 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha amesema viongozi wa dini nchini Tanzania wamekua ndio msingi wa Amani iliopo nchini.

Ameongeza kusema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini hapa nchini katika kuwaletea wananchi maendeleo husasani katika sekta za elimu na afya hasa katika maeneo ya pembezoni ya nchi.

Ametaja mchango wa kanisa la Orthodox nchini ambao ni pamoja na ujenzi Kliniki 90 pamoja na Hospitali katika mkoa wa kagera na shule katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na kanisa la Orthodox hapa nchini pamoja na dini zingine katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake Baba Mtakatifu Beatitude Theodoros II amesema amefurahishwa kushiriki mazungumzo na Makamu wa Rais na kumuomba kufikisha salamu zake kwa Rais Samia ambaye amemtaja kama mfano wa upendo unaopatikana nchini Tanzania.

Amesema Tanzania ni nchi imara sana ambayo amekua akiitaja katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo alipofanya ziara nchini Russia na kukutana na Rais wa nchi hiyo Vladmir Puttin.

Alipoulizwa juu nchi imara barani Afrika aliitaja Misri ikifuatiwa na Tanzania.