Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 14Article 546940

Habari Kuu of Wednesday, 14 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dunia yamkumbuka Mkapa

Dunia yamkumbuka Mkapa Dunia yamkumbuka Mkapa

VIONGOZI wanne wa kimataifa wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, leo wanashiriki kwenye mdahalo wa kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, utakaofanyika mkoani Dar es Salaam.

Viongozi hao watakaoshiriki kwa njia ya mtandao mdahalo huo ni aliyekuwa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ukimwi (UNAIDS), Winnie Byanyima.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Dk Ellen Senkoro, mdahalo huo umeandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na serikali.

Dk Senkoro alieleza kuwa mdahalo huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City ni sehemu ya kuenzi mchango wa Rais Mkapa kwa taifa, Afrika na duniani, na utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Hayati Benjamin Mkapa: Mwaka Mmoja Tangu Atutoke, Tunayakumbuka Maisha Yake, Tunaenzi Urithi Wake.”

“Mgeni rasmi katika siku hii muhimu anatarajiwa kuwa mpendwa wetu Rais Samia ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki kupitia uwepo wao binafsi au kwa njia ya mtandao,” alifafanua Dk Senkoro.

Alisema viongozi hao wanne wa kimataifa ambao ni Clinton, Blair, Obasanjo na Byanyima watatoa salamu zao kwa njia ya video wakielezea walivyomfahamu hayati Mkapa katika kushirikiana naye katika kazi na masuala ya kuleta maendeleo duniani hususan Afrika na nchini Tanzania.

Aliwataja viongozi wengine wa kitaifa watakaohudhuria mdahalo huo kuwa ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi, viongozi wakuu wa serikali, marais na viongozi wastaafu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini.

Wengine ni wakuu wa mashirika ya kimataifa nchini, wakuu wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi, wanafamilia na marafiki wa hayati Mkapa kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na asasi za kiraia na viongozi wa dini.

Alisema pia kutakuwa na mdahalo kuhusu mada isemayo “Afya kwa wote: Urithi wa Rais Benjamin Mkapa katika kujenga Mifumo ya Afya imara na endelevu.”

Alisema kupitia mada hiyo washiriki watapata fursa ya kusikia mjadala jinsi Mkapa alivyofanikiwa katika kuimarisha mifumo ya afya kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania popote alipo anapata fursa ya kupata huduma za afya.

“Mjadala huu pamoja na mambo mengine utashirikisha jopo la wadau watakaochambua kwa undani umuhimu wa uwekezaji katika mifumo imara ya afya na namna Tanzania ilivyopiga hatua katika eneo hili,” alisema Dk Senkoro.

Aidha, alibainisha kuwa pia leo Rais Samia atazindua mfuko maalumu wa taasisi “Endowment Fund” unaoanzishwa chini ya Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa lengo la kuongeza chachu katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Mdahalo utaanza saa 1.30 na unatarajiwa utamalizika saa 7.30 mchana. Alisema washiriki katika mdahalo ni wale waliopelekewa mialiko ambao wengi wao watashiriki moja kwa moja, na wachache wao pamoja na Watanzania wote watashiriki kwa kufuatilia mdahalo huu kupitia vyombo vya habari vitakavyorusha matangazo haya moja kwa moja.

Benjamin William Mkapa aliyeiongoza Tanzania kuanzia Novemba 23, 1995 hadi Desemba 21, 2005, alifariki dunia Julai 23, mwaka jana. Lakini tukio hilo la leo linafanyika wiki moja kabla ili kuipa nafasi familia na ndugu wa karibu kumuenzi mpendwa wao kwa hiyo siku alipofariki.