Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 13Article 546817

Habari Kuu of Tuesday, 13 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

EAC yazindua mpango kuibeba sekta binafsi

EAC yazindua mpango kuibeba sekta binafsi EAC yazindua mpango kuibeba sekta binafsi

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) ambayo ni taasisi inayounganisha vyama vya sekta binafsi Afrika Mashariki, wamezindua mpango maalumu wa kuimarisha sekta binafsi.

Kundi la Wataalamu (TWG) litakuwa na wanachama kutoka EAC na EABC imekusudiwa kuweka mikakati itakayonufaisha sekta binafsi katika Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mkuu wa Forodha na Biashara wa EAC, Kenneth Bagamuhunda, ataongoza TWG.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa TWG, Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki alisema EAC-EABC ina jukumu maalumu la kukuza shughuli ambazo zitaongeza kujulikana kwa EAC pamoja na kutoa jukwaa la kushughulikia changamoto zitakazobainishwa na wafanyabiashara katika ukanda huo.

Dk Mathuki alitaka TWG kumfikia kila mfanyabiashara, iwe mkubwa au mdogo, kwa kuweka nambari ya simu ya kupokea mawazo kutoka kwa wadau.

Alisema lengo la EAC ni kufanya sekta binafsi kuwa kitovu cha mchakato wa mtangamano ujumuishaji kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisisitiza kuwa kufanya kazi ya pamoja na umiliki itakuwa muhimu kwa mafanikio ya TWG ambayo inapaswa kuzingatia matokeo.

“Chochote tunachofanya lazima kitasababisha kitu kinachoonekana,” alisema Dk Mathuki, akiongeza kuwa hatua tatu za mtongamano wa EAC ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Fedha zilikusudiwa kukuza ujumuishaji wa kiuchumi katika ukanda huo.

“TWG inapaswa kuja na mfumo uliooanishwa wa majibu ya pamoja kwa nchi washirika kupambana na Covid-19 katika ukanda huo, suluhisho la pamoja katika eneo hili litawezesha kufufuliwa kwa uchumi baada ya Covid,” alisema.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga alisema sekta binafsi kwa kutumia TWG itakuwa imeshika nafasi yake katika mtangamano.

“Sekta binafsi kupitia EABC inapaswa kufanya kazi kwa karibu na Bunge ili kuhakikisha kwamba mfumo muhimu wa kisheria inawekwa kuwezesha maendeleo ya sekta binafsi Afrika Mashariki,” alisema Ngoga akiongeza kuwa ushirikiano kati ya EAC na EABC utasababisha mchakato wa mtangamano wa EAC kwenda hatua nyingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, John Bosco Kalisa alisema TWG itabaini masuala yanayozuia usafirishaji huru wa bidhaa katika ukanda huo na kutatuliwa kila mwezi.