Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 559132

Habari Kuu of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Familia yapoteza ndugu saba ndani ya siku 10

Familia yapoteza ndugu saba ndani ya siku 10 Familia yapoteza ndugu saba ndani ya siku 10

WATU saba wa familia moja wamepoteza maisha kwa kipindi cha siku 10, wakiwamo watano waliofariki dunia jana kwenye ajali ya gari iliyohusisha gari ndogo na lori wakitokea mkoani Mbeya walikokwenda kuhudhuria maziko ya ndugu yao.

Tukio hilo lilitokea jana eneo la Inyala mkoani Mbeya, watu watano wakifariki dunia, akiwamo mtoto.

Mmoja wa wanafamilia, Bupe Mboya, aliiambia Nipashe jana kuwa alipata taarifa ya ajali hiyo jana asubuhi ikiwa ni wiki moja tangu aliporejea kutoka mkoani Mbeya kwa mazishi ya mmoja wa wanafamilia.

“Baada ya kuzika Mbeya, ndugu yetu ambaye alifariki dunia Dar es Salaam na kusafirisha, imepita wiki moja, tulio wengi tulirudi na Costa kuja Dar baada ya maziko.

"Tukamwacha Tom (marehemu) na ndugu wengine wakisema watafuata siku chache baadaye kwa gari ndogo.

“Waliofariki dunia wote ni familia moja. Hapa nipo na mke wa marehemu kwa ajili ya kupanga safari ya kurudi tena Mbeya kwa mzishi kwa sababu miili ya marehemu imehifadhiwa Mbeya,” alisema Bupe.

Alibainisha Septemba 13, mwaka huu, yaani siku tisa zilizopita, familia hiyo ilipoteza mmoja wa wanafamilia na kuzikwa mkoani Dar es Salaam.

Aliendelea kusimulia kuwa Septema 15, mwaka huu, alifariki dunia mwanafamilia mwingine na kwamba wawili hao walikuwa wagonjwa hadi umauti unawafika.

“Siku 10 yaani haizidi wiki moja alifariki ndugu yetu na tulizika Kurasini. Baada ya siku tatu, tarehe 15 akafariki dada wa huyu tuliyemzika Kurasini.

"Huyu dada ndiye tulimsafirisha kwa ajili ya maziko na wakati wanafamilia tukirudi Dar es Salaam, ndugu zetu wakapata ajali na kufariki watano leo (jana)," alisema.

Kwa mujibu wa Bupe, ndugu waliofariki dunia jana kutokana na ajali hiyo ni: Thomas Mboya; Isabela Mboya; Joyce Mboya; Magreth Masaka; na Seviline Mgalla.

Jana mchana, Nipashe ilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alidai hakuwa na taarifa za ajali hiyo inayodaiwa kusababisha vifo vya ndugu hao.

Hata hivyo, majira ya saa 12 jioni, kiongozi huyo wa polisi alibainisha kuwa jeshi hilo lilikuwa linaandaa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.